Mkude awaachia msala wanne Simba

New Content Item (1)
New Content Item (1)

BAADA ya mabosi wa Simba kumsimamisha, Jonas Mkude kwa tuhuma za utovu wa nidhamu, kiungo huyo fundi ameachia msala viungo wengine wanne wanaocheza nafasi hiyo kikosini, huku Kocha Sven Vandenbroeck akisisitiza kazi inaendeleza bila hata nahodha huyo wa zamani.

Sven alisema kosa lililomuadhibu Mkude, lipo kiuongozi zaidi, ila kwa upande wake anaandaa atakayefiti kuziba nafasi ya kiungo huyo bila kuonyesha upungufu wowote na kutamba kikosi chake kina wachezaji 28, kwa maana anasaliwa na wengine 27 kikosini.

“Kukosekana kwake ni sawa kama amepewa kadi nyekundu, kuumia au kuwa na tatizo lingine la kumweka yeyote nje, hivyo bado tuna wengine wa kufanya kazi,” alisema Sven na kuongeza;

“Ukiangalia mechi iliyopita dhidi ya Majimaji na michezo mingine Mkude alikosekana na kuna waliocheza vizuri nafasi hiyo, hivyo tumefanya maandalizi ya kutosha na yeyote kati ya viungo nilionao ataziba nafasi hiyo ili tupate matokeo mazuri zaidi.”

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Kauli hiyo ya Sven ina maana kwamba Erasto Nyoni, Mzamiru Yassin, Said Ndemla na nyota mpya Taddeo Lwanga aliyesajiliwa dirisha dogo ndio walioachiwa msala wa kuziba pengo la Mkude, aliye mwandamizi ndani ya kikosi cha Simba.

Sven alisema tayari amejulishwa na viongozi kila kitu juu ya Lwanga kimekamilika ndio maana walisafiri naye kwenye mechi dhidi ya FC Platinum na kwamba alishindwa kumtumia kwa vile alipatwa na mafua na kumpumzisha na hata katika mechi yao ya Kombe la ASFC dhidi ya Majimaji waliyoifumua 5-0 hakumtumia, ila alisema;

“Kama hali yake itakuwa sawa na atafanya mazoezi vizuri nilipanga kuanza kumtumia katika mchezo dhidi ya Ihefu (uliopigwa jana) na ile ya marudiano dhidi ya Platinum.”

Juu ya adhabu ya Mkude, nyota wa zamani wa klabu hiyo na Yanga, Amri Kiemba akizungumzia suala la Mkude kwa utovu wa nidhamu, alisema sio tatizo kwa upande kiutawala, ila kiufundi walitakiwa kumpeleka timu ya vijana ili aendelee kujifua awe fiti zaidi.

“Kama angeendelea kufanya mazoezi na timu ya vijana ufiti wake usingeondoka kwa urahisi wakati mambo ya kiutawala yanaendelea na siku ambayo wangemrudisha katika kikosi angekuwa fiti kama kawaida lakini kwa hilo ambalo wameliamua upande wa kiufundi halitakuwa vizuri,” alisema Kiemba aliyewahi kucheza na Mkude kabla ya kwenda Stand United.