Mkichokoza tu...Yanga inatua hapa

KAMA uchokozi wa Simba utaendelea na wakala wa Bakary Mwamnyeto akizingua, Yanga imetamba itabeba mabeki wawili matata sana.
Uongozi wa Yanga kupitia kwa mdhamini wao GSM na Coastal Union wamemalizana kuhusu dili la Mwamnyeto lakini inadawa staa huyo amegoma kusaini mkataba wa awali na Yanga mpaka wakala wake ambaye yuko Italia afike.
Lakini wakala huyo, Kassa Mussa ameliambia Mwanaspoti Simba wamempigia kumpa ofa mpya ya Mwamnyeto ndio maana amemwambia mchezaji huyo asiwe na mzuka atulie kwanza.
Lakini Yanga baada kuona sintofahamu hiyo wakaona isiwe shida wameandaa mbadala. Tena mmoja wa wanayemtaka wanadai ndiye anayefuta makosa ya Mwamnyeto pale Coastal.
Yanga imeanza mikakati ya kuwasajili mabeki wawili, Ibrahim Ame wa Coastal Union na Dickson Job wa Mtibwa Sugar endapo dili la Mwamnyeto litabuma kutokana na tamaa ya pesa.
Mmoja wa viongozi wa Yanga, aliihakikishia Mwanaspoti jana wamefikia hatua nzuri sana kwa Mwamnyeto na kilichobaki ni kusaini kandarasi tu, lakini taarifa ya Simba kuingia tena imewafanya kuanza kufikiria wachezaji wengine ambao wanaweza kucheza nafasi hiyo kwani thamani ya Mwamnyeto inakuzwa sana na wao hawawezi kutoa Sh100 milioni.
“Tumeanza kuchukua tahadhari kuhusiana na suala la Mwamnyeto, mazungumzo yanakwenda vizuri, lakini sasa tunasikia kuwa meneja (wakala) wa mchezaji huyo pia amezungumza na Simba na kuwaambia wakutane na uongozi wa Coastal Union.”
“Hapa kuna kizungumkuti, sisi kama Yanga hatujui maendeleo ya Coastal Union na Simba pamoja na ukweli kuwa Coastal Union ina ofa yetu na mambo tulivyopanga yafanyike, tunawasikilizia wao,” alisema kiongozi huyo.
Alisema kuwa kiufundi Ame ni beki mzuri na hata bechi la ufundi la Yanga limevutiwa naye na kazi iliyobaki ni kuona jinsi gani wanamaliza majadiliano fasta na kuendelea na michakato mingine.
“Ame yupo katika makaratasi yetu na kama mambo yataenda vizuri, tutaanza mazungumzo rasmi, hii inakuwa siri ya klabu, lakini nia ipo na kama taasisi kubwa, lazima tuchukue tahadhari mapema,” alisema.
Kuhusiana na Job, kiongozi huyo alisema kuwa mchezaji huyo mbali ya kuwa na uwezo mkubwa, pia amepata uzoefu wa kimataifa kwani amecheza kuanzia timu ya u-17, U-20 na pia kuitwa katika timu za Taifa.
Alisema kuwa hawana shaka na uwezo wa Job na kwa sasa kama ilivyokuwa kwa Ame wanaanza mikakati ya kukutana na uongozi wa Mtibwa Sugar, meneja (wakala) wake na kufuata taratibu za kisheria.
“Yanga haitasajili mchezaji kiujanja ujanja eti kwa kuvizia ukiukwaji wa mikataba kwa sababu ya kutolipwa mishahara ya miezi mitatu au la, sisi ni taasisi kubwa na tunataka kujenga uhusiano na timu nyingine,” alitamba kigogo huyo na kudai msimu ujao watanoga sana.
Kwa upande wake,Job alisema kuwa yupo tayari kujiunga na timu yoyote ambayo itafuata masharti ya usajili. “Yanga nasikia tu, lakini bado sijafanya nao mazungumzo, kuna meneja wangu na uongozi wa klabu ambao wana mamlaka katika masuala ya usajili,” alisema Job.