Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Matheo Anthony: Kutoka ukonda, benchi Yanga hadi staa Polisi Tanzania

KILA mtu ana historia yake nyuma kila anapopiga hatua moja mbele kimaendeleo na ndivyo ilivyo kwa straika wa Polisi Tanzania, Matheo Anthony.

Kuna mambo mengi ambayo mashabiki na wadau wa soka hawayafahamu kuhusu straika huyo aliyepambana kuwania namba kwenye kikosi cha kwanza cha Yanga. Hata hicho alichemka na kuamua kwenda kusaka changamoto mpya na kulinda kipaji chake ndipo akatua zake Polisi Tanzania.

Lakini, unafahamu kuwa Matheo ni kama amedandia gari kwani, soka kwenye maisha yake hakukuwa na hesabu za kutoboa kimaisha kupitia soka.

Soka kwake halikuwa sehemu ya kumuingizia kipato, bali aliona ni kama kujifurahisha na kuujenga mwili wake kimazoezi.

Sio kwamba alikuwa haupigi mwingi, la hasha jamaa anajua na kuwa wakati alikuwa akikodishwa kwenda kucheza ndondo mitaani na hapo ndio akanogewa na kujikita ametuliza mizuka huku ndugu na jamaa wakimpa moyo kuendeleza kipaji na kulifanya soka kuwa sehemu ya maisha yake.

Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Matheo, ambaye amefunguka mambo kibao ikiwemo historia ya maisha yake na hapo linakufunula kila kitu.

ALIKUWA KONDA WA DALADALA

Tofauti na mastaa wengine wanapotoboa kimaisha huficha historia zao na mahali walipotoka, hilo kwa Matheo ni tofauti kabisa. Anaeleza kuwa kabla ya kujikita kwenye soka alikuwa kondakta wa daladala kule Zanzibar na ndio ilikuwa ikiendesha maisha yake.

Aliifanya kazi ya konda kwa mwaka mzima kuanzia 2013/14 na anakiri kwamba, haikuwa ikimlipa kiasi cha kuweka malengo ya maisha, lakini kwa wakati huo alikuwa akiitegemea.

“Baada ya kumaliza darasa la saba, nilianza kuangalia maisha ya baadaye… kila anayefanya kazi anajua malipo yake. Nilifanya kazi ya ukonda kwa mwaka mmoja, nilipata pesa ya kula na kufanya matumizi madogo madogo. Wakati huo nilikuwa nacheza sana ndondo kwa kukodishwa.

“Soka sikulifanya sehemu ya maisha yangu ingawa nilikuwa nikiingia uwanjani kucheza mashabiki wananishangilia na kunipa pesa nje ya ile ambayo nimekodishwa.

“Wakati nacheza mtaani kama kujifurahisha kuna kiongozi wa KMKM aliniona akanipenda nakutaka nichezee timu yake, alitumia muda mwingi kunishawisha kubadili kazi yangu ya ukonda,” anasema.

USAJILI WA KMKM

Mwaka 2014 alijiunga rasmi na KMKM na kuaminiwa baada ya mwalimu kumuingiza moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza bila kujali ametokea kwenye kazi gani kwani, kipaji chake ndio kiliongea kila kitu kuhusu yeye.

Wakati huo Matheo aliona kama zali kwani, ndicho kipindi ambacho alishika pesa nyingi tangu kuzaliwa Sh 2 milioni. Bila kupoteza muda alianza kuwekeza kwenye ujenzi wa nyumba yake.

“Kipindi hicho ndio ilikuwa pesa yangu kubwa, ikanipa moyo kuona soka linalipa tofauti na awali ambapo na hapo nikaingia kwa miguu yote,” anasema.

MIAKA MITANO YANGA

Unaambiwa mwenye bahati habahatisha ndivyo yalivyo katika maisha ya Matheo, pale KMKM alikaa mwaka mmoja kisha wababe wa Tanzanoa Bara, Yanga wakamuona na kurusha ndoana. Mwaka 2015 aliupiga mpira mwingi kwenye Kombe la Kagame, ambapo aliibeba KMKM kwenye mabega yake kwa kuonyesha soka la kuvutia.

“Baada ya mashindano yale, nikasajiliwa na Yanga na ndani ya kikosi hicho nilipata changamoto nyingi ikiwemo ya kukaa benchi. Sikuwa na namba ya kudumu na nilikuwa Napata nafasi ndogo sana ya kucheza mara kwa mara.

“Nilitamani kuaminiwa lakini, ilishindikana na nikawa nakaa sana benchi, kuna wakati nilikuwa nasahau kwamba kuna kucheza,” anasema Matheo.

Hata hivyo, anakiri licha ya kusugua benchi lakini, Yanga imempa mwanga wa maisha kwa kuwa amepiga hatua kubwa kimaendeleo.

“Yanga ni klabu kubwa, licha ya kuondoka kuna vitu nimefanya kupitia Yanga, sikujutia kuondoka kwani, kuna vitu navikumbuka,” anasema.

NIYONZIMA, ABDUL ACHA KABISA

Anasema wakati anasugua benchi, Haruna Niyonzima, Oscar Joshua na Juma Abdul walikuwa wakimpa moyo kwamba, ipo siku atacheza kwa mafanikio makubwa na kuwa mfano kwa wengine.

“Sitawasahau katika maisha yangu, hawa jamaa walikuwa walinipa moyo na ndio maana nipo Polisi Tanzania kwa sababu waliniaminisha kuwa muda wangu utafika na sasa umefika kweli,” anasema.

DILI LA POLISI TZ SASA

Kutua kwake Polisi Tanzania kumenusuru kiwango chake msimu ambapo, anapata nafasi kikosi cha kwanza na anaangaliwa kama mchezaji muhimu.

“Kitendo cha kuangalia wenzangu wakicheza na wakati huo nikiwa nimekaa kwenye benchi kinaondoa kujiamini na kushusha morali ya kujituma, hivyo najisikia furaha kutua Polisi Tanzania ambako nacheza,” anasema Matheo ambaye kwa sasa anamiliki ndinga yake tofauti na wakati ule akitoafuta kutoboa na kuwa konda.

0000