Mamilioni yatumika kuivuruga Yanga

Muktasari:
Mishahara ya wachezaji wote wa Coastal Union, chakula na kambi kwa mwezi ni wastani wa Sh.30 milioni. Straika Mnigeria Abasirim Chidiebele ndiyo mchezaji wa gharama zaidi katika kikosi cha Coastal analipwa Sh.2milioni huku Yanga anayelipwa zaidi anakinga Sh6 milioni.
BAJETI ya mishahara na kila kitu ya Yanga kwa mwezi ni Sh120milioni ambazo ukizipeleka pale Coastal Union zitatumika kulipa mishahara ya miezi minne na chenji itabaki.
Mishahara ya wachezaji wote wa Coastal Union, chakula na kambi kwa mwezi ni wastani wa Sh.30 milioni. Straika Mnigeria Abasirim Chidiebele ndiyo mchezaji wa gharama zaidi katika kikosi cha Coastal analipwa Sh.2milioni huku Yanga anayelipwa zaidi anakinga Sh6 milioni.
Mnigeria Chidiebele ndiye anadaiwa kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha ambazo ni Sh10milioni. Mkenya Tonny Otieno ambaye kwa sasa yuko kwao akiugulia majeruhi na kiungo Mcameroon, Sabo Yussouf wao wanashika nafasi ya pili kimshahara ambapo wanalipwa Sh 1.6milioni kila mmoja.
Wachezaji wengine wanalamba Sh600,000 na wengine Sh500,000 huku wachache wakipokea Sh 300,000. Pia inatumia wachezaji wa kikosi cha pili chini ya miaka 20 ambao inadawaiwa wanaishi kwa posho ya Sh 70,000 kwa mwezi lakini kula na kulala ni juu ya klabu.
Awali katibu mkuu wa klabu hiyo, Kassim El Siag alisema Coastal imepunguza sehemu kubwa ya bajeti ya klabu kwa mwaka huu tangu walipoanza kupanga nyumba kwa ajili ya kambi ya wachezaji na chakula.
Kwa sasa wamepanga nyumba kubwa mbili za kambi ya wachezaji, kila moja inalipiwa Sh360,000 kwa mwezi. Chakula inanunua klabu na kingine kinatoka kwa wadhamini, wana mpishi wao ambapo gharama kwa mwezi mzima ni sawa na Sh4milioni.
Bajeti ya Yanga kwa mwaka inakadiriwa kuwa Sh3bilioni. Bado Yanga inaongoza ligi na pointi 39 sawa na Azam lakini wao wana mabao mengi ya kufunga 36 wakati wapinzani wao hao wana 30, Yanga imefungwa mabao saba na Azam imefungwa 10.
Mechi ilivyokuwa Mkwakwani
Yanga ilitua Tanga kwa kujiamini lakini iliadabishwa kwa kucharazwa mabao 2-0 na kufanya mashabiki, wanachama na viongozi waliofurika uwanjani hapo kutoka vichwa chini kwa aibu.
Japo Yanga ililianza pambano kwa nguvu yake na kasi lakini wenyeji wao waliwadhibiti vilivyo hadi washambuliaji nyota, Amissi Tambwe na Donald Ngoma kuonekana wa kawaida.
Walidhibitiwa vilivyo na Adam Miraji dogo aliyesajiliwa kwa mkopo akitokea Simba na Hamad Juma aliyemnyima pumzi Ngoma muda wote wa mchezo huo uliosisimua.
Kutokana na Coastal kufanya mashambulizi ya mara kwa mara, beki wa kati wa Yanga, Kelvin Yondani aliyekuwa akihaha pande zote na kuziba mapungufu mengi yaliyotokea kushoto anakocheza Oscar Joshua, alijikuta akinawishwa mpira mkononi na mwamuzi Andrew Shamba kuamuru ipigwe adhabu.
Yule kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ ambaye alikuwa na jeuri ya kutofungwa bao, alishangaa mpira huo ukimpita tobo bila hata kujijua.
Kipindi cha pili Yanga ilirudi na kasi kwa lengo la kusawazisha lakini, ndoto yao ilizimwa dakika ya 62 baada ya Juma Mahadhi kupachika bao la pili lililowaamsha mashabiki wa Coastal.
Hali hiyo iliwafanya wachezaji wa Yanga wacheze kwa hofu kwani hawakuwa na maamuzi, timu ilipokuwa inafika ndani ya 18, walijikuta mipango yao inagoma, kiujumla ni kama walipaniki na ilijidhihirisha wazi dakika ya 75, Ngoma na Tambwe walijikuta wenyewe wakigombea mpira mmoja ambao pia lilikuwa ni bao la wazi.
Dakika zilivyozidi kuyoyoma, ndivyo wachezaji wa Yanga walivyoziid kuwa watumwa wa Coastal kwa kuwaokotokea mipira kwa sababu walikuwa wanachelewa kwenda kupiga na kurusha.
Hivyo hivyo, kwenye kuumia, wachezaji wa Coastal walikuwa wakigalagala sana uwanjani kwa madai ya kuchezewa vibaya, wakawa wanapoteza muda jambo ambalo liliwapa hasira wachezaji wa Yanga.
Hali hiyo ilisababisha dakika ya 89, Yondani atolewe kwa kadi nyekundu baada ya kumrushia daktari wa Coastal, Kitambi Mganga deli lake nje ya uwanja ili waendelee na mpira na daktari huyo alitahamaki na kumjibu na ndipo Shamba akamaliza ugomvi kwa kuwapa kadi nyekundu wote wawili.
Kutokana na kasi ya mchezo huo, Shamba alijikuta akivunja kadi nyekundu aliyokuwa amempa kiungo Mcameroon wa Coastal, Sabo Youssouf akijua ni Said Jeilan.
MAPENGO YAONEKANA
Yanga iliingia uwanjani hapo bila beki wake wa kushoto Haji Mwinyi na nahodha Nadir Cannavaro waliobaki Dar es Salaam wakisumbuliwwa na majeraha na nafasi zao zilizibwa na Oscar Joshua na Mtogo Vincent Bossou.
Walipokuwa Tanga, kiungo Mnyarwanda Haruna Niyonzima na Malimi Busungu waliugua malaria na wakatupwa jukwaani kuungana na winga, Godfrey Mwashiuya na kipa Benedictor Tinocco.
Kutokana na hali ya Uwanja wa Mkwakwani kuwa tofauti na ule wa Taifa, wadau wengi wanashauri wale ndiyo walistahili kucheza mechi hizo za mikoani kwa sababu wana uzoefu nazo kwani Mzimbawe Ngoma na Mrundi Amissi Tambwe huwa mara kwa mara wanachemka kwenye viwanja vya aina hiyo.