Majina 10 ya Pablo moto mpya Simba

Friday May 20 2022
Pablo PIC
By Thobias Sebastian

SIMBA ilipunguzwa kasi katika mbio za kutetea taji lao la Ligi Kuu baada ya sare ya 1-1 kwenye Uwanja wa Azam Complex na kuwaacha Yanga wakihitaji pointi tisa tu kutwaa ubingwa, lakini Wekundu hao wa Msimbazi tayari wameanza plani za kutisha za msimu ujao na pia kumaliza msimu huu kibabe kwa kuwafunga Yanga katika nusu fainali ya Kombe la ASFC jijini Mwanza.

Mabosi wa Simba wamempa rungu la kufanya uamuzi kocha wao, Pablo Franco juu ya nyota wapya ambao atakuwa anawahitaji kwa ajili ya msimu ujao na wale atakaopendekezwa waachwe kama ilivyokuwa kwa Bernard Morrison.

Katika kuhakikisha hilo linakwenda vizuri tayari Pablo amewasilisha ripoti yake yenye mahitaji ya kiufundi huku akiwa kuna baadhi ya wachezaji wapya anaotamani kuwa nao msimu ujao akiendelea kuwafuatilia.

Taarifa za ndani zinaeleza Pablo ana majina ya wachezaji zaidi ya kumi kutoka katika timu tofauti wakiwamo wazawa na wageni na kati ya hao kuna watakaopewa mikataba ya kujiunga na Simba msimu ujao.

Kwenye orodha hiyo ya Pablo kuna wachezaji kutoka Asec Mimosas, wengine Afrika Kusini huku miongoni mwa wazawa waliokuwemo wapo, Cleophas Mkandala wa Dodoma Jiji na Aziz Andambwile wa Mbeya City.

Wengine ni nahodha wa Biashara United, Abdulmajid Mangalo, beki Dickson Mhilu wa Kagera Sugar, Nathan El Chilambo wa Ruvu Shooting na wengineo ambao Pablo anaendelea kuwafuatilia kabla ya kufanya uamuzi ya kuwasajili kati ya hao.

Advertisement

Kwenye orodha hii ya wachezaji wazawa Pablo amevutiwa nao ila bado wapo kwenye mchujo, huku Mkandala, Mangalo, Mhilu na Chilambo mwisho wa msimu mikataba yao inamalizika kwenye timu wanazocheza.

Simba msimu huu wamepanga kuboresha kikosi chao kwa kuongeza wachezaji wa kigeni si chini ya wanne wanataokuwa wa kikosi cha kwanza moja kwa moja pamoja na nguvu nyingine ya nyota wazawa.

Wakati hilo likiendelea mabosi hao wa Simba wanaendelea kuzungumza na baadhi ya wachezaji wao wanaomaliza mikataba ili kuwaongezea mikataba mipya kwa ajili ya kuendelea kukipiga Msimbazi kama kipa, kipa Aishi Manula.

Kwenye nyakati tofauti viongozi wawili wa juu Simba, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Salim Abdallah ‘Try Again’ na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez walieleza nyota wao muhimu wanaonamiza mikataba hawataondoka kwani watawaongezea mingine pamoja na kumpatia kila anachohitaji Pablo kwa ajili ya msimu ujao.

Kwa upande wa Meneja wa Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally alisema kuhusu usajili Wanasimba wasiwe na wasiwasi hakuna mchezaji wanayemtaka ataondoka.

“Ukiona mchezaji yoyote kasajiliwa na timu ya humu ndani kutoka Simba basi jua hakuwa kwenye mipango yetu,” alisema Ally kupitia mtandao wake wa Instagram.


MECHI YA AZAM

Azam walipata bao la kuongoza katika dakika ya 37 kupitia kwa Rodgers Kola akifunga katika nyavu tupu kumalizia mpira uliorudishwa ndani na Daniel Amoah.

Kola, ambaye pia ndiye aliyefunga bao la kufutia machozi kwa kubinuka tiktaka katika mechi ya raundi awali ya ligi Januari mosi mwaka huu ambayo Simba ilishinda 2-1, hakuweza kuendelea na mechi jana kwani aliumia kwa kujigonga na nguzo ya lango wakati akifunga na nafasi yake kuingia Shaaban Idd Chilunda.

Simba ilijibu mpigo kwa bao zuri la John Bocco katika dakika ya 44 akiunganisha kwa kichwa frii-kiki tamu ya Shomari Kapombe.

Mbali na kuwaadhibu waajiri wake wa zamani, Bocco aliboresha mwendo wake mzuri wa kutupia, akifunga katika mechi yake ya tatu mfululizo ya Ligi Kuu, baada ya kuanza msimu vibaya na kumaliza raundi 21 za kwanza za mechi bila ya kufunga bao.

Baada ya kosakosa za kipa upande, Azam walilalamikia kunyimwa penalti katika dakika ya 58 baada ya Kibu Denis kushika mpira kwa mikono miwili aliyoiinua juu wakati akijaribu kuokoa mpira lakini mwamuzi Elly Sasii alimeza filimbi.

Advertisement