Maisha ya Salah Stamford Bridge yalivyokwenda kombo

Muktasari:
- Salah aliwahi kuichezea Chelsea kati ya mwaka 2013 hadi 2016 lakini mambo hayakwenda sawa. Unajua ni maisha gani aliyokumbana nayo Chelsea?
STAA wa Liverpool, Mohamed Salah jana Jumapili alirejea katika uwanja wake wa nyumbani, Stamford Bridge akiwa ni Mwanasoka Bora wa England msimu huu huku akisubiri kutwaa kiatu cha dhahabu na kuwa Mfungaji Bora wa Ligi Kuu ya England.
Salah aliwahi kuichezea Chelsea kati ya mwaka 2013 hadi 2016 lakini mambo hayakwenda sawa. Unajua ni maisha gani aliyokumbana nayo Chelsea?
UWEZO MKUBWA
Chelsea ilithibitisha kumsajili Mohamed Salah, Januari 27, 2014 akipewa jezi namba 15, ujio wake ukitoa nafasi kwa Juan Mata kujiunga na Manchester United. Kabla ya kutua Chelesa, iliripotiwa kuwa Liverpool nayo ilimfukuzia, lakini Chelsea ikaibuka kidedea katika mbio za kuwania saini yake, baada ya kuvutiwa na kiwango chake, walipokutana na Basel kwenye mechi ya Europa.
“Ni mdogo, ana kasi, ni fundi, uwezo ni mkubwa sana, ana ari ya kucheza mpira lakini pia ana mvuto akiwa uwanjani,” hii ilikuwa ni kauli ya Kocha wa Chelsea, Jose Mourinho akimzungumzia Salah wakati huo na kuongeza :
“Tunaamini tukiwa na Salah, Andre Schurle, Eden Hazard, Oscar na Willian, tutakuwa sawa. Tunampoteza mchezaji muhimu kama Juan Mata, lakini tunashukuru kumpata kinda huyu mwenye uwezo mkubwa.”
DALILI ZA TATIZO?
Mechi ya kwanza ya Salah katika kikosi cha Blues, ilikuwa ni dhidi ya Newcastle United. Mechi hii ilipigwa Februari 08, ambapo Chelsea ilikula 3-0, huku Salah akiingia akitokea benchi katika kipindi cha pili. Mechi yake ya pili, ilikuwa ni sare ya 1-1 dhidi ya Brom siku chache baadaye. Dalili za kutokea kwa tatizo katika uhusiano wa Salah na Mourinho, zilianza kujionesha katika mchezo wa FA ambapo Chelsea ilipigwa 2-0 na Man City. Mourinho alisikika akihoji mchango wa Salah kikosini. Nyota huyu, aliingia kuchukua nafasi ya Samuel Eto’o lakini uwepo wake uwanjani haukuleta mabadiliko yoyote katika jahazi la Chelsea ambalo lilikuwa linazama. Mourinho katika mazungumzo na waandishi alisikika akisema Salah, aliyeigharimu Pauni milioni 16, bado hayuko tayari kuichezea Chelsea.
“Hakuwa mchezoni dhidi ya Man City, ana kasi lakini bado sana. Anahitaji muda wa kuimarika, bado hajasoma aina ya uchezaji wa klabu, hili ni tatizo. Kucheza Stamford Bridge sio sawa na kucheza Basel,” alisema Mourinho.
“Unapoichezea klabu kama Basel, unacheza kujifurahisha tu, kule hakuna presha. Ukija hapa, lazima upate presha kwa sababu kwanza unatazamwa na mashabiki zaidi ya 40,000, kila mtu anakuangalia wewe. Nadhani Salah anahitaji miezi sita ya kuzoea mazingira,” aliongeza wakati huo.
Mreno huyo, alikiri kuwa awali alikuwa na imani na Salah na kuongeza kuwa msimu uliofuata Mmisri huyo angeonesha makali yake. Hata hivyo, hilo lilisalia kuwa ndoto kwani baadaye alipelekwa Fiorentina kwa mkopo.
SWAHIBA WA BENCHI
Salah hakufanikiwa kuingia dimbani katika michezo sita iliyofuata. Mourinho alimfanya aanzishe urafiki na bechi ya Chelsea. Salah alirejea uwanjani katika ushindi wa 6-0 dhidi ya Arsenal, akitupia bao moja wavuni. Hii ilikuwa ni mechi ya 1,000 ya Arsene Wenger, akiwa Kocha wa Arsenal.
Ilimchukua dakika nne tu, baada ya kuingia uwanjani, katika kipindi cha pili, akichukua nafasi ya Oscar, kuitungua Arsenal, akitumia vyema uzembe wa mabeki wa The Gunners.
Mourinho alishangilia sana na kumwagia sifa mchezaji huyu. Alinukuliwa akisema: “Bao hili ni muhimu sana kwake, bado ni mdogo, ni mtoto, kama ataendelea kufunga itamsaidia kujenga hali ya kujiamini. Anahitaji uungwaji mkono na ulinzi kutoka kwetu, tutamlinda.”
NYOTA WA MCHEZO
Kiwango cha Salah kiliendelea kuimarika siku hadi siku. Baada ya muda mrefu wa kusubiri hatimaye, Aprili 05, 2014, Salah alipata nafasi kikosi cha kwanza cha Chelsea.
Katika mechi hiyo, Salah alionesha uwezo mkubwa na kuibuka mchezaji bora wa mechi huku akifunga bao moja katika ushindi wa 3-0 dhidi ya Stoke, pale Stamford Bridge. Mmisri huyu alifunga bao la kuongoza, kabla ya kuizawadia Chelsea penalti iliyopigwa na Frank Lampard, kabla ya kumpenyezea Willian mpira na kufunga bao la tatu. Alipoulizwa kuhusu kiwango cha Salah, Mourinho alijibu: “Nadhani hatukosea kumsajili. Tulimuuza Mata, tukampata kinda, watu walishangaa, lakini leo tumeshuhudia, alipata nafasi kwenye kikosi cha kwanza, akathibitisha uwezo wake, tumeshinda,” alisema Mourinho
“Kuna aina mbalimbali ya mawinga, kuna wanaopenda kukaa na mpira, lakini kuna wengine kama Salah wanapenda kutembea nao, wanapenda kuweka mpira kwenye mstari, hapa hatukukosea.”
SAFARI YA KUONDOKA ILIANZIA NORWICH
Chelsea ilikuwa katika mbio za kuwania ubingwa wa EPL, waliposafiri kwenda kuikabili Norwich. Mourinho akamuamini Salah, akampanga katika kikosi cha kwanza. Hata hivyo, mechi hii, ndio iliyofungua milango ya kuondoka Stamford Bridge kwa winga huyu. Mourinho hakuridhishwa kabisa na kiwango kilichooneshwa na Salah, akamtoa uwanjani katika kipindi cha kwanza. Baadaye alisikika akisema, “Kipindi cha kwanza kilikuwa kibovu, wachezaji walikuwa wazembe sana, hakuna kasi, hakuna ari ya kupata ushindi, bure kabisa.”
JINAMIZI LA NEW MEADOW
Salah alihusika katika mechi zote za kujiandaa na msimu mpya wa ligi wa 2014/15. Alifunga mabao katika mechi za kirafiki dhidi ya AFC Wimbledon na Vitesse Arnhem, lakini ligi iliopoanza, mambo yalianza kumuendea kombo. Matumaini yote ambayo Mourinho yakayeyuka. Salah alikuwa chaguo la tano, asingepata namba mbele ya Hazard, Schurrle, Willian na Oscar. Mara chache alizopata nafasi, ilikuwa dhahiri kuwa, alipoteza uwezo wa kujiamini na hivyo alipoteza mipira kiholela. Katika mchezo wa Kombe la ligi dhidi ya Shrewsbury Town, uliopigwa New Meadow, Salah hakuwa na jipya lolote. Alipiga shuti moja ambalo hata hivyo lilitoka nje. Muda mfupi alitolewa uwanjani. Hii ilikuwa ni siku mbaya zaidi katika maisha ya soka ya winga huyu. Chelsea ilishinda 2-1, lakini Mourinho alighadhabika sana na kiwango cha nyota huyo na wenzake.
“Huwa nategemea wachezaji kunipa presha, napenda sana kupata matatizo kutoka kwao, lakini hawa wala hawajanipa tatizo lolote, sijapata kigugumizi cha kupanga kikosi na sitokaa nipate tatizo la kuamua nani acheze. Kama kwenye mechi ya awali wachezaji waliocheza dakika 90 walionesha kiwango kikubwa, nategema wachezaji waliokaa benchi wawe na hasira ya kuthibitisha uwezo zaidi ya niliowapanga, lakini kwa hawa hamna kitu,” alisema.
NI WAZI ANAONDOKA
Salah aliingia katika mechi mbili tu baadaye. Mechi yake ya mwisho ikiwa ni katika mchezo wa raundi ya tatu, Kombe la FA ambapo Chelsea ilipigwa 4-2 na Bradford, Stamford Bridge. Hii ilikuwa ni Januari 24, 2015. Wiki moja baadaye, Salah alijiunga na Fiorentina kwa mkopo, huku Juan Cuadrado akitimkia Stamford Bridge. Katika miezi yake 12, aliyochezea Chelsea, aliingia dimbani mara 19 tu.
Akiwa Italia, nyota ya Salaha iling’ara, katika mechi saba za mwanzo alitupia wavuni mara sita. Huu ulikuwa ni mwanzo wa safari ya mafanikio kwa nyota huyu wa Liverpool. Kuanzia hapo alikwenda Roma kwa mkopo kisha ikamnunua jumla. Kiwango chake kikaenda juu zaidi na zaidi mpaka Liverpool ikaamua kumrudisha katika Ligi Kuu ya England. kilichobaki kwa sasa ni historia.