Madaktari waonya kina Molinga kuongezeka uzito

Dar es Salaam. Kocha msaidizi wa timu ya soka ya Yanga, Charles Mkwasa, juzi alianika ripoti ya vipimo vya madaktari wa timu hiyo vinaonyesha kuwa baadhi ya wachezaji wameongezeka uzito akiwamo mshambuliaji anayeongoza kwa mabao kikosini, David Molinga.
Kufuatia ripoti hiyo, baadhi ya madaktari wa michezo wameonya na kuwataka wachezaji hao kupunguza uzito kwa kuwa una athari mbalimbali katika uchezaji na maisha yao.
Mbali na Molinga aliyeongezeka kwa kilo 12, Mkwasa alimtaja Yikpe Gislain kuwa na kilo 10, Said Makapu kilo sita na Patrick Sibomana aliyeongezeka kilo saba.
“Ripoti ya timu ya madaktari inaonyesha baadhi wachezaji walikiuka maagizo waliyopewa, hivyo kujikuta wakiongeza uzito,” alisema.
“Programu maalumu tulizowapa zilikuwa na maelekezo, kuna baadhi hawakuzifuata na kabla ya mambo mengine tumewapa programu nyingine ya kupunguza uzito.”
Hii siyo mara ya kwanza kwa Molinga mwenye mabao manane ambaye ni kinara wa ‘kucheka’ na nyavu Jangwani msimu huu kuelezwa kuongezeka uzito kwani hata kocha aliyepita, Mwinyi Zahera aliwahi kumlalamikia.
Madaktari waonya
Wakizungumzia suala la mchezaji kuongezeka uzito kuelekea kuanza mechi, madaktari wameonya kuwa inaweza kuwa na athari.
Daktari wa Yanga, Shecky Mngazija alisema siku zote kilo za mchezaji zinapaswa kulinganishwa kwa uwiano wa uzito na urefu.
“Uzito wa Balama (Mapinduzi) na Lamine (Moro) lazima uwe tofauti kutokana na maumbile yalivyo ya wachezaji hao. Ili kurejesha kilo (za kawaida) wanatakiwa kupunguza kula vyakula vya wanga, protini na sukari, wafanye mazoezi wakiwa wamevaa mavazi maalumu ya kukata uzito,” alisema Mngazija.
Alisema moja ya vitu ambavyo vinasababisha mtu kuongezeka uzito ni pamoja na kula vyakula vingi vya wanga, protini na sukari pamoja na kupumzisha mwili kwa muda mrefu kwa kutoushughulisha.
Kwa upande wake, Dk Shita Samwel alisema mchezaji anaongezeka uzito kutokana na kushindwa kufanya mazoezi na kula zaidi. “Mchezaji anapoongezeka uzito lazima apungue kasi yake (uwanjani) kwa sababu anakuwa na uvivu na hawezi kufanya mazoezi kwa wepesi,” alisema.
Naye daktari wa Azam FC, Mwanandi Mwankemwa alisema wanaoongezeka uzito wanajiweka hatarini kupata magonjwa kama shinikizo la damu na kupooza na ni rahisi kupoteza maisha.
“Mtu anapoongezeka uzito ni rahisi kupata pia ugonjwa wa kisukari na mbaya zaidi ugonjwa huu unaathiri figo, mishipa ya fahamu, mishipa ya damu na vilevile macho yanaathirika,” alisema.
Nini kifanyike
Dk Shita ambaye pia ni tabibu wa wanamichezo, anasema ili kupunguza uzito ni lazima mchezaji apate ushauri wa wataalamu lishe wa michezo ambao wanaweza kumpangia aina ya lishe anayopaswa kuitumia, vinginevyo itakuwa vigumu kurejea haraka katika uzito wa kawaida.
Hata hivyo, Dk Mwankemwa alisema muda uliobaki kabla ya ligi kuanza wachezaji hao wanaweza kupunguza uzito kama watafuatilia kwa makini maelekezo ya wataalamu.
Yanga mwishoni mwa wiki ijayo itakuwa ugenini kucheza na Mwadui FC kwenye Uwanja wa Kambarage mjini Shinyanga katika mfululizo wa michezo ya Ligi Kuu Bara.
Katika msimamo wa Ligi Kuu Bara, Yanga inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 51, ikiwa nyuma ya Simba inayoongoza yenye pointi 71 na Azam FC iliyo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 54.