Lwanga aanza kazi Simba SC, amtaja Mkude

Lwanga aanza kazi Simba SC, amtaja Mkude

Dar es Salaam. Kiungo mpya wa Simba, Taddeo Lwanga amefanya mazoezi kwa mara ya kwanza na timu yake mpya kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena tangu ilipocheza mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Plateau United.

Lwanga aliyesajiliwa wiki iliyopita alisema alikuwa akiifutialia timu hiyo vya kutosha na kubaini kuna wachezaji bora katika kila nafasi moja.

Alisema ukiangalia kikosi cha Simba si nafasi ya kiungo mkabaji, ambayo anacheza, kuna wachezaji bora katika maeneo yote, kila mchezaji ana uwezo wa kufanya kazi iliyokuwa bora kulingana na majukumu ya nafasi hiyo.

“Nimeona Simba kuna viungo wengi wazuri na hadi unapata nafasi ya kucheza katika kikosi cha kwanza au kuingia kuna kazi kubwa.

“Ukiangalia katika mechi na Plateau, nafasi ya kiungo mkabaji walicheza Jonas Mkude na Mzamiru Yassin, ambao walitimiza majukumu vizuri, lakini ukiachana na hao kuna viungo wengine kama Said Ndemla na Larry Bwalya hawakutumika na wapo katika viwango bora.

“Ubora wa viungo na wachezaji wote wa Simba unalifahamu hilo na nipo tayari kwa kushindana na kuna kitu ambacho nitajitahidi ili kuongeza katikati ili kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kwani wote tuna malengo ya kuifikisha timu mbali.

“Katika mechi ya Plateau ambacho nimekuona mchezo ulikuwa wa mbinu zaidi ndiyo maana hata mashambulizi hayakuwa mengi kwa upande wetu, kwanza tulitaka kulinda bao ambalo tulipata ugenini, lakini kuhakikisha pia tunamaliza dakika 90, na matokeo ambayo yangetuvusha.

“Shida ambayo niliiona Plateau walipata nafasi moja ya kufunga ile ya dakika ya mwisho, ambayo kwetu ilituweka katika wakati mgumu mno, ila makosa yameonekana na kocha ataturekebisha,” alisema Lwanga, ambaye amesajiliwa kuwa mbadala wa Mbrazil Gerson Fraga.

Lwanga hatakuwa na kazi rahisi kupenya katika kikosi cha kwanza cha Simba na kupewa nafasi ya kucheza katika nafasi ya kiungo mkabaji kwani kwa miaka tisa ambayo Mkude amedumu, alionyesha kujihakikishia namba.

Kama hiyo haitoshi, Simba imewahi kuwa na viungo wakabaji wazuri waliosajiliwa kwa nyakati tofauti kama, Justine Majabvi, James Kotei na Gerson Fraga, lakini Mkude amekuwa akipata nafasi ya kucheza mbele yao au wanatumika wote kwa pamoja.

Miamba hiyo itashuka katika mchezo wa Ligi Kuu kesho kuivaa Polisi Tanzania.

BY Thobias Sebastian