Lavagne: Tukishinda tu ugenini baasi

Mabosi na benchi la ufundi la Azam tayari wamepata faili la wapinzani wao kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, Al Akhdar ya Libya huku wakitamba kulijua vyema soka la Afrika.

Azam itaanzia ugenini Oktoba 8, mwaka huu na mechi ya marudiano itakuwa nyumbani jambo lililompa nafasi kocha mkuu wa Matajiri hao wa Chamazi, Mfaransa Denis Lavagne kutumia uzoefu wake wa soka la Afrika kuwaondosha Walibya hao na kutinga hatua ya makundi.

Kocha huyo aliyewahi kucheza fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 2008 akiinoa Cotton Sports ya Cameroon na 2021 alipoifikisha JS Kabaiyle ya Algeria fainali ya Kombe la Shiriisho ameeleza kulijua vyema soka la Afrika na kuwasoma Al Akhdar.

“Utamaduni wa soka la Afrika kwa kiasi kikubwa unafanana, kwenye michuano hii kila timu inahitaji ushindi nyumbani na Al Akhdar wako hivyo,” alisema Lavagne na kuongeza;

“Sio timu ya kubeza, nimewaona wako vizuri lakini tunahitaji kupata matokeo chanya kwenye mechi zote mbili, tunajua ugenini itakuwa mechi ngumu zaidi lakini tumejipanga kuhakikisha tunashinda.”

Azam ni timu pekee ya Tanzania iliyoanzia hatua ya kwanza kwenye michuano ya CAF msimu huu na inatarajia kuondoka nchini katikati ya wiki hii kwenda Libya kwaajili ya mchezo wa kwanza utakaopigwa Oktoba 8, 2022 kuanzia saa 2:00 usiku kwenye Uwanja wa Martyrs of February.

Mechi ya marudiano itakuwa kati ya Oktoba 14-16 kwenye Uwanja wa Azam Complex.