Lampard apiga simu Bayern Munich akimuulizia Alaba

Saturday June 27 2020
alaba pic

LONDON, ENGLAND. CHELSEA imeripotiwa kuwasiliana na Bayern Munich kuulizia mpango wa kwenda kunasa huduma ya beki wa kushoto David Alaba wakati dirisha la usajili wa majira ya kiangazi litakapofunguliwa.

Kocha wa Chelsea, Frank Lampard anatarajia kuingia sokoni kusaka huduma ya beki wa kushoto kuja kukipiga kwenye kikosi chake kwa msimu ujao, huku Emerson Palmieri na Marcos Alonso wakitarajia kufunguliwa milango ya kutokea mwishoni mwa msimu.

Beki wa kushoto wa Leicester City, Ben Chilwell amekuwa akihusishwa na mpango wa kwenda kutua katika kikosi cha The Blues, lakini bei ya staa huyo wa kimataifa wa England imeripotiwa kuwa kubwa na kumfanya Lampard kufikiria mara mbili.

Kwa mujibu wa The Athletic, Chilwell ndiye chaguo la kwanza la Chelsea kwenye nafasi ya beki ya kushoto, lakini wamefungua milango ya kutazama mabeki wengine na hapo wanacheki namna ya kumchukua Alaba.

Ripoti zinadai Chelsea wamewasiliana na Bayern kuwauliza mabingwa hao wa Ujerumani kama wapo tayari kumuuza beki wao huyo kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.

Barcelona, Real Madrid na Inter Milan nazo zimekuwa zikimtolea macho beki huyo, ambaye mkataba wake huko Allianz Arena utafika kikomo mwisho wa msimu ujao.

Advertisement

Alaba, amecheza mechi 380 za michuano yote kwenye kikosi cha Bayern Munich, ikiwamo 36 katika msimu huu na sehemu kubwa alitumika kama beki wa kati.

Advertisement