KUOMOKA NAYO, ENGINEER OLUNGA NA PESA ZAKE

STRAIKA matata wa Harambee Stars ambaye anazidi kuomoka kila kukicha, Michael ‘Engineerí Olunga tayari ameanza kula maisha kule Qatar.

Hii ni baada ya kukamilisha uhamisho uliogharamu Sh1 bilioni kutoka Kashiwa Reysol ya Japan League 1, kujiunga na mabingwa wa Qatar Al-Duhail SC.

Uhamisho wake ulizua mjadala mkubwa nchini miongoni mwa mashabiki, wachanganuzi wa soka na wadau mbalimbali wa soka nchini. Wapo waliohisi haukuwa uamuzi mzuri kitaaluma kwenda Qatar na wapo waliosapoti uamuzi huo kwa sababu ungemfanya aomoke.

Kwa wachache wengi waliosapoti uhamisho huo, suala la kuomoka ndilo lililotawala mawazo yao likiwa ndio kiini kikubwa wanachoamini ndicho kilichompelekea kukubali ofa hiyo.

Wenye mawazo hayo, waligonga ndipo, kwani kulingana na wandani wa karibu wa Olunga, fowadi huyo aliyekulia maisha yake ya utotoni katika mitaa ya mabanda mjini Nairobi, aliamua kuomoka kwanza kisha mengine yatafuata.

Kwa maana hiyo ulikuwa ni uamuzi mwepesi kwake kufanya. Aliamua akimbizane na pesa kwanza na kama ni masuala ya taaluma, hiyo itakuwa stori ya siku nyingine.


ACHOREA GIZA OFA YA BILIONEA WA MISRI

Watu wake wa karibu wameidokezea safu hii kuwa kabla ya dili la Al-Duhail SC kuja, tayari kulikiwa na ofa aliyokuwa amewekea mezani na bilionea kutoka Misri.

Wadokezi hao wameifahamisha safu hii kwamba bilionea Turki Al Sheikh anayemiliki klabu ya Pyramids yenye makao yake mjini Cairo, alikuwa tayari kamwekea ofa Olunga, miezi sita kabla ya Alh-Duhail kujiongeza kwenye mix ya kuiwinda sahihi yake.

Kulingana na ofay a Al Shiekh, bwanyenye huyo alikuwa tayari kumlipa Olunga mishahara wa Sh12 milioni kila mwezi, kwa mkataba wa miaka mitatu.

Hata hivyo Olunga aliamua kuichorea giza sababu kubwa ikiwa ni suala la ubaguzi wa watu weusi kule Misri na kupendelea kwenda Qatar ambako kuna idadi kubwa ya wazalendo wenzake Wakenya. Lakini pia marupurupu na bonasi zilichangia

Kando na ofa a Al Shiekh, pia Olunga alipokea ofa nyingine kutoka klabu moja ya Saudi Arabia ila Engineer alipendelea zaidi kwenda Qatar.


QATAR ATALAMBA SH16 MILIONI KWA MWEZI

Safu hii pia imebaini kuwa kabla ya kukubali ofa ya Al-Duhail, Engineer aliomba mshahara aliomkuwa akipokea Kashiwa Reysol, uongezwe kwa asilimia 100%. Pale Kashiwa mshahara wake kwa mwezi ulikuwa Sh8 milioni. Al-Duhail inayomilikiwa na bwanyenye Abdullah bin Nasser Al Ahamed, ilikubali kuongeza mshahara wake kwa asilimia fulani. Lakini ili kutumiza alichouliza, klabu hiyo ilifanyia maboresho bonasi na marupurupu yake. Bonasi na marupurupu hayo atalipwa kutegemea na magoli atakayofunga lakini pia, matokeo yatakayozalishwa na timu kwa ujamla.


MILIONI YA KWANZA AILAMBIA SWEDEN

Baada ya kuimbuka mchezaji bora katika msimu wa 2015 akiwa na Gor Mahia, aliitiwa majaribio katika klabu ya Sweden. Olunga alijiunga na Gor kwa uhamisho wa Sh200,000 akitokea Tusker na kuibuka mfungaji bora msimu huo kwa magoli 19.

Ndipo klabu ya IF Djurgardens ilimwalika kumfanyia majaribio. Alifanyiwa majaribio kwa muda wa mwezi mmoja na kuishia kusainiwa kwa mkataba wa kudumu uliomlipa mshahara wake wa kwanza katika kiwango cha milioni na zaidi. Awali Gor ilitaka asiondoke ila Olunga akaitisha mshahara wa Sh1.5 milioni kwa mwezi. Gor haikuwa na uwezo huo hivi ikamwachia.


WACHINA WAMPA SH12 MILIONI KWA MWEZI

Kule Sweden, Olunga alitia sahihi mkataba wa miaka minne lakini aliutumikia kwa mwaka mmoja pekee kabla ya kunyakuliwa na Wachina. Baada ya mwanzo mgumu, Olunga alifanikiwa kumaliza msimu wake wa kwanza na IF Djurgaden kwa kupachika magoli 12 katika mechi 13 alizocheza.

Ubora wake ukaivutia klabu ya Guizhou Hengfeng iliyoamua kumsajili kwa kuvunja dau la mkataba alilokuwa amewekea na klabu hiyo ya Sweden. Hengfeng ililipa IF Djurgardens Sh500 milioni kama fedha za uhamisho wa Olunga baada ya kuvunja kipengele hicho.

Olunga akasaini nao mkataba wa miaka minne uliokuwa ukimlipa Sh12 milioni kila mwezi. Pia Hengfeng ilimlipa Olunga Sh288 milioni zikiwa ni fedha za sign-on fee-malipo apewayo msanii baada ya kukubali kusajiliwa kukwingine. Alitumikia mkataba wake hadi ulipofikia kikomo na ndipo Kashiwa Reysol wa Japan waliamua kumchukua 2018, timu ikiwa daraja la pili.


MSHAHARA JAPAN SH8 MILIONI

Pale Reysol alitia saini mkataba wa miaka mitatu. Ni mkataba uliomlipa mshahara wa Sh8 milioni kila mwezi. Kwenye msimu wa kwanza aliwasaidia kupandishwa daraja baada ya kufunga magoli 28.

Msimu wa mwaka jana, Olunga aliibuka mfungaji bora wa ligi kuu ya Japan J1 League kwa kupachika magoli 28 vile vile.

Alilipwa Sh529,000 kwa kuibuka na kiatu hicho cha dhahabu. Lakini pia, Olunga alilipwa kiasi kingine zaidi Sh1 milioni baada ya kutawazwa mchezaji bora wa msimu 2020.

Kaondoka mkataba wake ukiwa umesalia na mwaka moja baada ya Al-Duhail kufika bei.


Imeandikwa na Thomas Matiko