Kipre, Akaminko waigawa Yanga

WAKATI sakata la kiungo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ likiendelea kutikisa nchini, uamuzi wa mabosi wa Yanga kuandika barua Azam FC ili kuwaulizia nyota wawili wa timu hiyo winga, Kipre Junior na kiungo, James Akaminko, limewagawa baadhi ya wadau wakiwamo nyota wa zamani wa Jangwani.

Yanga iliuandikia uongozi wa Azam kuulizia juu ya mikataba yao na kama wanapatikana ili wasajiliwe kwenye dirisha dogo na mabosi wa Azam umeshawapa majibu kwamba hawana noma, lakini wadau hao wamegawanyika baadhi kuona kama ni kiini macho na siasa za soka la Bongo.

Uongozi wa Yanga uliandika barua iliyosainiwa na Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Andre Mtine, ikiwa siku chache tangu Fei Toto alipoilipa Yanga Sh 112 milioni za kuvunja mkataba na kulipa mishahara ya miezi mitatu kwa madai ya kutumia vipengele vya mkataba wake na Yanga.

Fei alitoa fedha hizo kabla ya kuaga mashabiki wa Yanga kwa madai ya kutaka awe huru na kutafuta changamoto sehemu nyingine kutokana na fedha nyingi ambazo amewekewa katika mkataba na kilichofanywa na Yanga kuwataka kina Akaminko imeonekana kama ni kutaka kulipa kisasi.

Hata hivyo, nyota na kocha wa zamani wa Yanga, aliyekuwa akiinoa Ruvu Shooting msimu huu kabla ya kujiengua, Charlse Boniface Mkwasa alisema haoni shida kama sajili hizo zitafanyika kwani kila mchezaji anapenda kuichezea klabu kubwa ambayo itamtangaza zaidi.

“Ni fursa kwao ila kikubwa hata hao wachezaji waangalie huko wanakoenda watapata nafasi kama ambavyo walikuwa wanapata mwanzo isije ikawa sababu ya wao kushindwa kuonekana na vipaji vyao kupotea,” alisema Mkwasa, huku Edibily Lunyamila alisema kwa upande wake anaona ni siasa ambazo kwa kiasi kikubwa zinatumika kuwapoza mashabiki kutokana na suala la Feisal kwani kwake haoni kama ni usajili muhimu.

“Nikiangalia kikosi kimejitosheleza sana ila shida pekee bado ni kwenye michuano mikubwa ya kimataifa sasa kama wanaleta wachezaji ambao hawawezi kutumika kwangu naona haina manufaa kwao zaidi ya siasa tu,” alisema winga huyo wa kimataifa wa zamani wa Biashara Shinyanga, Yanga, Malindi Simba na Taifa Stars.

Kwa upande wake, Sekilojo Chambua ambaye pia amewahi kupita Yanga alisema yeye ni mshabiki wa Kipre Junior na anatamani kumuona akitua Yanga, ingawa viongozi wanapaswa kuangalia wachezaji wanaoweza kuwatumia kimataifa. Yanga ina wachezaji 12 wa kigeni kama kanuni inavyoruhusu na ilikuwa ikihaha kutafuta nafasi ya kutaka kumuongeza Yacouba Songne katika dirisha dogo, hivyo kama Azam itawapa baraka ya kuwasajili kina Akaminko, basi klabu hiyo italazimika kuwatoa nyota watatu walionao sasa. Lakini haitaweza kuwatumia nyota hao wa Azam kwenye mechi za makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, kwani walishatumika kwa vile walishaitumikia timu hiyo kwenye mechi za raundi ya kwanza.