GSM: Watakuja kwa bei yoyote

WAKATI sakata la kiungo Feisal Salum likiwa bado halijapoa, klabu ya Yanga imejibu mapigo kwa kuamua kugonga hodi ndani ya Azam FC kwa kutoa ofa ya kutaka kuwasajili nyota wawili wa timu hiyo, kiungo James Akaminko na winga Kipre Junior.
Inadaiwa mabosi wa Yanga wametuma ofa hiyo kwa Azam ikiwa siku chache tangu kuwepo kwa taarifa za kiungo Feisal Salum 'Fei Toto' kuvunja mkataba kwa kuilipa klabu hiyo Sh 112 Milioni ili awe huru na kukamilisha dili lake la kukipiga Azam iliyotajwa mapema kumnyemelea nyota huyo.
Yanga kupitia mfadhili wao GSM imedaiwa kutuma barua rasmi kwa Azam jana wakiwataka uongozi wa matajiri hao kuwapa bei ya wachezaji hao wawili haraka ili wafanye biashara.
Hatua hiyo ya Yanga ni kama kujibu mapigo kwa Azam ambao inatajwa kumshawishi Fei Toto  kuvunja mkataba na klabu hiyo ili ahamie Chamazi.
Mapema Mwanaspoti linafahamu kuwa tajiri wa Yanga, Ghalib Said Mohamed 'GSM' amekuwa shabiki mkubwa wa Akaminko ambaye amezidi kuwa na kiwango bora sambamba na Kipre ambao wote kwa pamoja walisajiliwa msimu huu.
Katika barua ambayo Mwanaspoti imeisoma kwa umakini, GSM anataka apewe bei ya wachezaji hao huku pia akiusisitiza uongozi wa Yanga chini ya Rais Hersi Said kukaa mezani na Azam ili Yanga iwapate wachezaji hao.
Endapo Yanga utampata Akaminko raia wa Ghana itaziba pengo la Feisal kirahisi endapo ataondoka klabuni hapo.
Mbali na barua hiyo Mwanaspoti linafahamu winga Bernard Morrison amepewa jukumu la kumshawishi Akaminko kukubali ofa hiyo ya Yanga.
Jana Mwanaspoti lilimtafuta Rais wa Yanga, Injini Hersi Said ambaye hakutaka kuliongelea hilo kwa undani akitaka utafutwe uongozi wa Azam.
"Nafikiri kama kuna kitu cha kusema sasa ni wakati wa Azam, ninachofahamu Yanga tumeshawishika sana na kiwango bora cha Kipre na Akaminko nadhani kila mtu anayejua soka amewaona," alisema Hersi, huku Mtendaji Mkuu wa Azam, Abdukarim Amin 'Popat' alikiri kupokea barua hiyo ya kutakiwa kwa wachezaji hao na kusema hawana tatizo watawajibu kwa kuwaainisha fedha wanazotaka.
"Sisi Azam FC hatuna mbambamba. Ni kweli tumepokea barua ya Yanga inayowataka kina Akaminko, tunaijibu kwa vile ni jambo zuri na sisi tupo tayari kufanya biashara nao," alisema Popat na kuongeza kuwa, Azam haina tatizo na kuwaachia wachezaji wake, kwani haitakuwa mara ya kwanza kwa klabu hiyo kufanya biashara  na Yanga, akigusia kuwapa Gadiel Michael na Salum Abubakar kwa vipindi tofauti, huku nayo ikiwanyakua Mrisho Ngassa, Frank Domayo na Didier Kavumbagu na nyota wengine wa Jangwani.