Kocha: Ahmada ni bonge la kipa mazoezini

KOCHA Mkuu wa Azam FC, Dani Cadena, amejitokeza hadharani na kumtetea kipa wa kikosi hicho, Ali Ahmada kutokana na kile kinachoonekana nyota huyo kufungwa mabao ya kizemba kwenye michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Bara.

Kipa huyo raia huyo wa Comoro, alishindwa kuokoa mpira vizuri uliopigwa na kiungo wa Yanga Stephane Aziz Ki na kumkuta Farid Mussa aliyeipatia Yanga bao la tatu na la ushindi wakati timu hizo zilipofungana mabao 3-2 katika mchezo wa Ligi Kuu wikiendi iliyopita.

Akizungumza na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Cadena alisema bado ana imani kubwa na kipa huyo kwani ndiye ambaye amekuwa akionyesha kiwango kizuri mazoezini hivyo suala la yeye kufungwa linaweza kumtokea yoyote yule.

“Mashabiki wanapaswa kutambua huu ndiyo msimu wake wa kwanza hapa Tanzania, hivyo siyo rahisi kuendana na mazingira kwa urahisi,” alisema.

“Hakuna anayependa kuona timu inafungwa kwani kosa lake linaweza kumtokea mchezaji yeyote hivyo nitaendelea kumjenga mazoezini kwa sababu binafsi naamini ni kipa bora kwetu na Tanzania.”

Wakati Cadena akimtetea nyota huyo taarifa zilizopo ni kwamba viongozi wa klabu hiyo walitaka kuvunja mkataba naye kutokana na kosa alilolifanya juzi na kwenye baadhi ya michezo iliyopita, lakini changamoto pekee ni kiasi cha fedha watakachotakiwa kumlipa.

Endapo Ahmada atavunjiwa mkataba wake wa miaka mitatu aliosaini na Azam FC basi viongozi watapaswa kulipa kiasi cha Dola 300, 000, ambazo ni Sh700 milioni, jambo ambalo ndilo linaloonekana dhahiri kuleta changamoto.

Ahmada mzaliwa wa Ufaransa alijiunga na Azam FC akitokea Klabu ya Sportsklubben Brann ya nchini Norway akiwahi kucheza timu mbalimbali Barani Ulaya ikiwemo miamba ya Ufaransa, Toulouse inayoshiriki Ligue 1.

Akiwa Toulouse ambayo alianza kuichezea timu ya vijana kuanzia mwaka 2009 na mwaka 2011 akapandishwa, alicheza jumla ya mechi 133 hadi anaondoka Ufaransa na kwenda Kayserispor ya Uturuki mwaka 2016 hadi 2019, kisha kuhamia Klabu ya Kongsvinger ya nchini Norway.