Kipa Azam: Kuna sehemu nimekosea
KIPA wa Azam FC, David Kisu hakuitwa kwenye kikosi cha Taifa Stars na sasa hajawa chaguo la kwanza la Kocha George Lwandamina ambapo yeye amekiri kushuka kwa kiwango chake.
Hiyo ndiyo sababu aliyoitaja kuwa imechangia kutoitwa Stars na kuondolewa kikosi cha kwanza cha Azam na kwamba sasa anapambana ili kurejesha kiwango chake.
Azam ilimsajili Kisu akitokea Gor Mahia ya Kenya akiwa mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika msimu uliopita.
Akizungumza visiwani hapa, Kisu alisema anaamini kiwango chake kitarejea kama kawaida kwani hali hiyo huwa inawatokea wachezaji wengi.
“Hata mimi najiona siko vizuri kwasasa, kuna vitu vimepungua lakini naamini nitarekebisha na kurudi kwenye ubora wangu, kiukweli najiona kuna vitu vimepungua kwangu,” alisema Kisu.
Akizungumzia mashindano ya Kombe la Mapinduzi, alisema kwao yamekuwa na changamoto kutokana na matokeo ya hatua ya makundi ambapo mechi ya kwanza walitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Mlandege.
“Kuna ushindani mkubwa na mbaya zaidi mechi ya kwanza pamoja na kutoka sare lakini hayakuwa matokeo mazuri kwetu kwani yalitupa wakati mgumu mechi ya mwisho.”
Mechi ya mwisho Azam walicheza jana Jumapili usiku na kushinda bao 1-0 na watacheza mechi ya kwanza nusu fainali ya kwanza dhidi ya Yanga SC leo jioni.