Kaze: Huyu Carlinhos noma!

Kaze: Huyu Carlinhos noma!

Muktasari:

  • Carlinhos hajaonekana katika mechi tano za Ligi zilizopita na mchezo wa mwisho kucheza kwake ni ule dhidi ya Coastal Union ambao Yanga ilishinda mabao 3-0 huku akifunga moja na kutengeneza lingine kikosi kikiwa chini ya kocha Zlatko Krmpotic.

YANGA inashuka uwanjani leo usiku kuikabili Namungo Jijini Dar es Salaam, lakini Kocha Cedrick Kaze ametamka Carlos Carlinhos ni kama gari limewaka.

Carlinhos hajaonekana katika mechi tano za Ligi zilizopita na mchezo wa mwisho kucheza kwake ni ule dhidi ya Coastal Union ambao Yanga ilishinda mabao 3-0 huku akifunga moja na kutengeneza lingine kikosi kikiwa chini ya kocha Zlatko Krmpotic.

Yanga chini ya utawala wa kocha Cedric Kaze kiungo huyo hajacheza mchezo wowote wa ligi zaidi ya kucheza mechi za kirafiki pekee.

Kaze ambaye ni Mrundi alisema Carlinhos amepona kabisa majeraha yake na sasa yuko sawa kuendelea na kazi na kuna vitu amegundua katika muda ambao wamekuwa akifanya mazoezi.

Kaze alisema anajua mashabiki wanafurahia ubora wa Carlinhos katika kupiga kona, krosi kali na hata mipira ya adhabu lakini kwake anaona raia huyo wa Angola ndio kiungo mwenye pasi za uhakika zaidi.

Kocha huyo alisema; “Najua mnaona Carlinhos anajua kupiga hiyo mipira tu,mimi namuona tofauti kidogo huyu ni hatari zaidi kwa pasi zake nafikiri anaweza kuwa ndio bora katika kupiga pasi zinazofika.”

“Kuna pasi ambazo mchezaji anapiga ambazo zinakwenda kuwamaliza wapinzani hizo zipo kwa Carlinhos katika muda ambao amefanya mazoezi nimeliona hilo,” alisema ambaye hajapoteza mchezo tangu atue Yanga na kuongeza;

“Alikuwa hayuko sawa kiafya lakini sasa amerejea kama ataendelea kuwa sawa atatusaidia sana kwenye timu naona kuna nafasi yake,”

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga Mhandisi Hersi Said amesema ukimya wa kiungo huyo wala hauwapi mashaka na muda si mrefu atarejea kazini.

Hersi ambaye ndiye aliyesimamia usajili wa kiungo huyo alisema baada ya kupata shida katika mambo ya vyakula sasa shida hiyo itakuwa imemalizika baada ya mkewe kuja nchini.

“Wakati anafika alikutana na changamoto mbalimbali kama kuzoea mazingira na hasa chakula, tulifanya juhudi za kutosha kumuokoa unajua huyu tusisahau ni mchezaji wa kwanza kutoka Angola kucheza hapa kwetu,” alisema Hersi.

“Baada ya hapo wakati anaanza kuzoea akapata majeruhi tena ambayo yakamkosesha mechi kadhaa na sasa amepona na ripoti tunayopata na kujionea pia yuko sawa.

“Hatuna wasiwasi naye na safari hii naona atarejea kwa nguvu zaidi kwa kuwa hata familia yake ipo hapa mke wake alifika hapa na wako hapa na unajua faida ya mtu wa mbali kuwa karibu na familia yake,” aliongeza.

......................................................

Na Khatimu Naheka