Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Kama vipi irudiwe

GEMU tamu sana. Wachezaji waliipenda na hata mashabiki waliipenda. Takwimu za dakika 90 zinaonyesha hakukuwa na butu butu nyingi ingawa rafu zilionekana.

Kila mmoja amelala salama. Hakukuwa na matokeo ya lawama kwa upande wowote. Kwa mara ya kwanza katika miaka ya hivi karibuni baada ya mechi ya watani, jana wachezaji, makocha wa Simba na Yanga baada ya mchezo walikumbatiana na kubakia uwanjani kwa dakika kadhaa wakipiga stori kuashiria ilikuwa ni gemu tamu kuwahi kutokea au kama vipi...irudiwe.

Ni mechi ya watani iliyomalizika kwa suluhu kwenye Uwanja wa Mkapa ambayo mashabiki hawakutarajia kutokana na mbwembwe zilizotawala nje ya uwanja kwa wiki kadhaa kuelekea mchezo huo.

Simba kama mwenyeji waliingia mchezoni wakiwa kamili na kuonekana kujiamini muda wote kama ilivyokuwa kwa Yanga ambao walitawala mchezo kwa mujibu wa takwimu za Azam Tv.

Mashuti yaliyolenga goli, Yanga mawili, Simba matatu. Yanga yaliyokosa ni matatu, Simba saba. Katika mchezo huo ulioshuhudia Yanga ikipiga kona nne dhidi ya moja ya Simba, mipira ya kuotea ilikuwa miwili kila upande.Kwa mujibu wa takwimu Yanga ilitawala mchezo kwa asilimia 51 dhidi ya 49 za Simba.

Kwa suluhu hiyo Yanga wanaendelea kubaki kileleni baada ya kufikisha pointi 20, wakati Simba watabaki nafasi ya pili na pointi zao 18.

Kipindi cha kwanza kilianza kwa timu zote kucheza kwa nidhamu kubwa katika kushambuliana kwa awamu pamoja na nidhamu kubwa kwenye kukaba na kuzuia ubora wa mpinzani wake.

Dakika 15 za mwanzo Yanga walicheza soka la chini na kutengeneza nafasi mbili za kufunga kwa aina tofauti ambazo zote walipoteza kupitia Fiston Mayele ambaye aliwazidi ujanja mabeki wa Simba na kufanya shambulio ambalo mpira wake ukifika nje, dakika tatu mbele walipata kosa iliyounganishemwa na kichwa cha Yanick Bangala kilitoka nje.

Simba dakika 15 za kwanza, walicheza soka lao la chini na kumiliki mpira na shambulio la hatari walilolifanya ni faulo ya Benard Morrison ambayo mpira wake ulikwenda kuwagonga mabeki wa Yanga.

Katika dakika hizi shida kubwa iliyoonekana kwenye timu zote, Simba walikuwa na shida kwenye kukaba hasa eneo la kiungo ambalo kazi hiyo kwa ukubwa alikuwa akifanya Jonas Mkude ambaye ilikuwa akipitwa lango la Simba linakuwa hatarini.

Yanga shida ilikuwa ni kukosa utulivu hasa kwenye eneo la kumalizia kwani walifika zaidi langoni mwa Simba na kutengeneza nafasi za kufunga na walishindwa kugeuza kuwa mabao.

Katika dakika 15 za pili Simba walifika langoni mwa Yanga kufanya shambulio la maana kupitia kwa Morrison dakika 28, ila mpira wake ulikwenda kuzuia na mabeki wa Yanga.

Yanga walifanya mashambulizi ya maana mawili yote kupitia kwa Mayele yote alishindwa kufanya kitu mbele ya mwamba, Henock Inonga ambaye alimzuia kwa mtindo wa ‘takolini’.

Simba wao waliimarika kwenye eneo la ulinzi walicheza kwa maelewano na kuwazuia Yanga vizuri, waliendelea kucheza soka la chini na kumiliki mpira kwa mrefu kwa kupiga pasi zao za chini wakianzia nyuma mpaka mbele.

Katika dakika 15, za mwisho Yanga walibadilisha aina yao ya uchezaji soka la chini pasi na kupiga mipira mirefu kutoka kwa Bakari Mwamnyeto au Bangala kwenda kwa Mayele.

Aina hiyo ya uchezaji iliipa faida Yanga, kwanza Mayele alikwenda kuwasumbua zaidi mabeki wa Simba ambao walikuwa imara kumzuia pamoja na kupata nafasi ya wazi ya kufunga dakika 43, kupitia kwa Mayele ambaye alipoteza mpira wa wazi baada ya kipa Aishi Manula kuteleza na kuacha mashabiki wakiwa mikono kichwani.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi zaidi upande wa Simba ambao walionekana kusaka bao kwani walifika zaidi langoni mwa Yanga kupitia kwa Morrison aliyepiga shuti kali ambalo lilikwenda katika mikono salama na Djugui Diarra.

Katika kuhakikisha wanaendelea kulisakama lango la Yanga, kocha wa Simba, Pablo Franco alifanya mabadiliko matatu katika nyakati tofauti walitoka Kibu dakika 63, Meddie Kagere, Benard Morrison na nafasi zao kuchukuliwa na John Bocco, Rally Bwalya na Yusuph Mhilu.

Mabadiliko hayo ya Simba, yalionekana kuwa na faida kwanza yalitimiza malengo ya benchi la ufundi kwenda kushambulia zaidi kwa kufanya mashambulizi ya mara kwa mara na kuwafanya Yanga kucheza kwa kujilinda tofauti na kipindi cha kwanza.

Yanga walifanya shambulizi moja la hatari kipindi cha pili lililokwenda kugonga mwamba baada ya shuti kali lililomshinda kipa, Aishi Manula kulizuia kwa namna yoyote ile.

Katika kuhakikisha wanamaliza na matokeo mazuri Yanga walifanya mabadiliko mawili alitoka Mayele na Moloko nafasi zao walichukua Makambo na Farsi Mussa.

Mpaka dakika 90, zilipomalizika timu hizo ziligawana vipindi Yanga walikuwa bora kipindi cha kwanza wakati Simba walikuwa imara katika kipindi cha pili.


MAKOCHA

Kocha wa Simba, Pablo Franco amewapongeza wachezaji wake kwa kucheza vizuri mchezo licha ya kwamba hawakuweza kupata ushindi huku akiipa tano zaidi safu yake ya ulinzi.

“Tulicheza vizuri katika baadhi ya vipindi lakini tulicheza vizuri zaidi katika safu ya ulinzi huku tukitumia mashambulizi ya kushitukiza, zaidi niwapongeze wachezaji wangu kwa juhudi kubwa waliyoionyesha katika mchezo huo,” alisema Pablo.

Kocha wa Yanga, Nasdreddine Nabi alisema Yanga ilikuwa bora na ndio maana walitengeneza nafasi nne za kufunga huku akikiri kuwa mechi ilikuwa ngumu.

“Kila timu iliingia uwanjani ikiwa 50/50 ya ushindi lakini tulicheza vizuri zaidi kipindi cha kwanza na karibu mechi nzima tuliizuia Simba kutengeneza nafasi ya magoli kwani nafasi ya wazi waliyopata ni moja tu ambayo iliokolewa na kipa Diarra,” alisema Nabi.

Kocha huyo alitamba kwamba Yanga inazidi kuimarika na ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu.