Kaburu aiburuza Simba TFF

Aliyewahi kuwa makamu mwenyekiti wa klabu ya Simba, Geodfrey Nyange 'Kaburu'.

ALIYEKUWA mgombea wa nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi mkuu wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, aliyekatwa jina lake ameliamsha baada ya kuiburuza Kamati ya Uchaguzi wa klabu hiyo kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) akikata rufaa dhidi ya uamuzi aliofanyiwa.

Uchaguzi wa Simba umepangwa kufanyika Januari 29 mwakani na Kaburu hajakubaliana na uamuzi wa kukatwa kwa jina lake na kukimbilia TFF kuitafuta haki wakati mchakato wa uchaguzi huo ukiendelea.

Mapema Kamati ya Uchaguzi ya Simba iliwaondoa wagombea mbalimbali wa mchakato huo wa uchaguzi akiwamo Kaburu katika mchujo wa awali na kubakisha wagombea 14 wakiwamo wawili wanaowania uenyekiti na 12 wa Ujumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa klabu hiyo.

Taarifa kutoka ndani ya TFF ambazo Mwanaspoti limejiridhisha ni kwamba Kaburu aliukatia rufaa uamuzi huo akiwa na hoja mbili kubwa akianza na uhalali wa kamati hiyo akidai haikuwa na sifa za kuendesha uchaguzi huo.

Hoja ya pili ya Kaburu ni kwamba ameeleza jinsi Kamati ya Uchaguzi ilivyomnyima haki yake kwa kutompa taarifa ya kwanini jina lake limeondolewa katika mchujo huo kitu ambacho anaamini hakikuwa halali.

Tayari rufaa hiyo imeshasikilizwa juzi katika makao makuu ya TFF na Mwanaspoti linajua kwamba wakati wowote uamuzi wa rufaa hizo utatolewa.

“Tumeshasikiliza hiyo rufaa ya Kaburu, subirini tu wakati wowote mtapewa majibu,” alisema mmoja wa wajumbe wa kamati iliyosikiliza rufaa hiyo.