Job afunika Yanga

Saturday November 27 2021
JOB PIC
By Mwandishi Wetu

KUNA beki Yanga kwa kuangalia kimo chake ni rahisi kusema hafai kucheza nafasi ya beki wa kati lakini makocha Wazungu wamekuwa wakikomaa naye na sasa ameshtua kwa rekodi ya maana.

Huyu ni Dickson Job na katika kipimo cha mabeki wanaoruka juu kwa haraka ameibuka kinara akiwashinda hata warefu kina Bakari Mwamnyeto.

Kocha wa mazoezi ya viungo wa Yanga, Helmy Gueldich amefichua kwamba Job mbali na kimo chake kutokuwa cha kuridhisha lakini sio rahisi kwa makocha kumweka nje kwa kuwa ndiye beki ambaye amekuwa mwepesi kuruka juu katika mipira ya vichwa.

Helmy alisema beki huyo amekua kinara katika timu yao akiwashinda hata wachezaji warefu ambapo hilo ndio limekuwa likimpa ubora anapokutana na washambuliaji warefu.

Job amekuwa beki anayewanyima usingizi washambuliaji warefu akiwemo nahodha wa Simba John Bocco ambaye rekodi zinaonyesha amekuwa akikutana na wakati mgumu anapokutana na beki huyo.

“Job ni kinara hakuna beki anayejua kuruka juu kwa haraka kama yeye msimuangalie kwa kimo chake,anajua sana kuruka hata nahodha Mwamnyeto (Bakari )hamfikii,nafikiri hicho ndio kitu kinachompa nafasi sana,”alisema.“Job pia anajua kuanzisha mashambulizi nafikiri mmekuwa mkimuona anafika mpaka eneo la mwisho la kushambulia ni bahati mbaya tu mpaka sasa hajafunga lakini kuna siku atafunga,duniani sasa wanataka mabeki wa namna hii.”

Advertisement

“Hata Mwamnyeto naye ameanza kuongezeka ubora zaidi naye ameongezeka sana ubora anaruka sana na anaanzisha mashambulizi kuna wepesi wameupata.” Kocha huyo alisema kwamba kama mchezaji huyo ataendelea na mzuka alionao atang’ara kwa kipindi kirefu.

Advertisement