Ishu ya kina Aziz KI, Okrah yawagawa mafaza

BODI ya Ligi (TPLB) juzi usiku ilitangaza mabadiliko ya kanuni ya usajili wa nyota wa kigeni kwa kusema wachezaji wote 12 wanaosajiliwa na timu moja wanaruhusiwa kucheza mechi moja, jambo lililowaibua wadau waliopokea kwa mitazamo tofauti.

Klabu kadhaa nchini msimu huu zimeshindana kusajili nyota wa kigeni huku baadhi yao wakianza kupata umaarufu mkubwa kama Stephane Aziz Ki, Gael Bigirimana, Augustine Okrah, Nelson Okwa, Kipre Junior, Tape Edinho na Ali Ahamada kabla hata Ligi Kuu Bara haijaanza kesho.

Badiliko hilo la kanuni kutoka klabu kuruhusiwa kusajili wachezaji 12 na kuwatumia nane tu katika mchezo mmoja na sasa kuruhusiwa wote, imewafanya wachezaji wa zamani kutoa maoni yao, baadhi wakiifagilia na wengine kuiponda.

Nyota wa zamani wa Reli Moro, Simba na Taifa Stars, Fikiri Magoso alisema wachezaji katika timu wanasajiliwa 30 hao 12 kutumika itawafanya wapiganie namba jambo ambalo litaongeza uhai katika timu.

“Mimi sioni shida hata kidogo hiyo itamfanya kila mchezaji kuzinduka kuhakikisha anaingia kwenye kikosi cha wachezaji 20 wanaosafiri na baadae kupambania 18 na mpaka 11,” alisema Magoso na kuongeza;

“Mimi bodi ya ligi naiunga mkono mpira sio mchezo wa kubebana itakuwa chalenji nzuri sana kwao hasa hawa wazawa ambao wanajisahau sana.”

Kocha wa Geita Gold, Fred Felix ‘Minziro’ alisema, wazawa hii fursa kwao kujituma na kujitambua wajibidiishe sana kwa kuwa mpira umekuwa ajira ndio maaana hata timu ndogo zinajitutumua kusajili wageni.

“Timu kubwa zina uwezo wa kununua wachezaji hao ila sisi timu ndogo kazi kubwa sana hata mimi naona kuwapa changamoto kina Zoran Maki wa Simba na Nasreddine Nabi wa Yanga napata kitu sana na kujiheshimisha,” alisema Minziro.

Peter Manyika, kipa wa zamani wa kimataifa wa Tanzania alisema, kuna upande mmoja ni sawa na mwingine sio sawa hasa katika timu ya taifa kuzidi kupoteza mvuto.

“Mimi naona ni sawa na sio sawa, kama wachezaji wetu wazawa wakijielewa itakuwa bora kwao, lakini wakiendelea kama walivyo kazi kubwa sana, maana wenye uwezo mkubwa wa kusajili wachezaji hao ni Simba, Yanga na Azam,’’ alisema Manyika, huku Abdallah Kibadeni alipinga kanuni hiyo kwa madai itapoteza uhai wa timu ya Taifa ambayo kwa asilimia kubwa inategemea wachezaji kutoka timu kubwa.

“Sio sahihi itawanyima kucheza hawa wachezaji wazawa na timu ya taifa itapata wapi wachezaji wazuri, kama wangesajiliwa 12 ila waruhusiwe watatu ingekuwa bora sana, lakini kwa 12 ni wengi sana, maana timu zinazotizamwa wachezaji wao kuitwa ni hizo zenye uwezo huo wa kusajili,” alisema Kibadeni.