Hii hapa siri ya Birthday ya mtoto wa Hamisa Mobetto

WADAU wengi wa burudani wamekuwa wakijiuliza swali hili na hata wewe unayeisoma habari hii si ajabu ukawa mmoja wa wanaojuliza hivyo.
Kwanini staa wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz, hakumfanyia ‘Birthday’ ya kifahari mwanaye Dylan aliyezaa na Hamisa Mobetto tofauti na anavyopanga kufanya huko Afrika Kusini kwa mwanaye mwingine, Latifa ‘Tiffah’ aliyezaa na Zari ‘The Boss Lady’.
Sasa kama unajiuliza swali hilo basi jibu lipo hapa na kama unamfahamu mtu mwingine anayejiuliza swali kama hilo, mwambie anunue Mwanaspoti tu ajipatie jibu.
Ishu nzima hapa inawekwa wazi na Hamisi Tale ‘Babu Tale’ ambaye ni meneja wa mwanamuziki huyo alipozungumza na Mwananspoti na kusema aliyesababisha Dylan afanyiwe sherehe ndogo ni Hamisa mwenyewe.
“Alikataa sherehe ya kifahari ambayo Diamond alitaka kuifanya, yeye (Hamisa) alitaka sherehe yenye maadili ya kidini,” alisema Babu Tale.
Aliongeza Hamisa alitaka sherehe ya kumbukumbu ya kuzaliwa ya mwanaye aliyetimiza mwaka mmoja, ishirikishe watoto yatima ikiwa ni sadaka kwa Mungu kwa jinsi anavyomjalia uhai na kumwombea makuzi mema.
“Hamisa alitoa sababu ya kufanya hivyo, alisema tangu mwanaye azaliwe amekuwa mtoto wa maneno maneno kwa watu, hivyo akaona bora akasherehekee na yatima ili kushukuru Mungu zaidi kwa mtoto alipofikia sasa,” aliongeza Babu Tale.
“Yaani alitaka siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Dylan iwe ya kufanya dua na kutoa sadaka, ndio maana mliona alipita katika ofisi za Wasafi TV kuja kukata keki, baada ya hapo akaenda kwa watoto yatima kumalizia sherehe ya mtoto.
“Sasa watu wasioelewa wanaona kama Diamond ameamua tu kutomfanyia sherehe Dylan.”
Birthday ya Tiffah aliyetimiza miaka mitatu siku chache zilizopita inatarajiwa kuwa bonge la pati na itafanyika hivi karibuni huku ikitarajiwa kuwakutanisha pia mastaa kadhaa.
Ampongeza Hamisa
Babu Tale hakuficha hisia zake aliposema kitendo alichofanya Hamisa ni kizuri na anampongeza kwa hilo.
“Unajua wakati mwingine mtu anapoamua maamuzi yake na yakawa mazuri kwa jamii, haina budi kumpongeza. Kwangu naona Hamisa alifanya jambo jema,” alisema.
“Kitendo cha kuamua kuwakumbuka watoto yatima na kushiriki nao katika kumbukumbu ya mwanaye kina thawabu kubwa sana kwa Mungu, nampongeza na wengine tuige mfano huu.”
Tuhuma za kumtenga Dylan
Babu Tale alipoulizwa kuhusu kinachoonekana WCB kumtenga mtoto wa Hamisa na kuwa karibu na watoto wa Zari (Tiffah na Nilan) hali wote ni wa baba mmoja, Diamond, alisema watu wanazungumza mambo wasiyoyajua.
“Hakuna kitu kama hicho katika familia ya WCB, yaani watu wangejua tulivyokuwa na upendo wala wasingekuwa wanasema hayo,” alisema.
“Hakuna ubaguzi wa aina yoyote, Dylan ni damu ya Diamond sasa kwanini atengwe? Hizo habari za mitandaoni tu.”
Afurahia kuitwa Mnafiki
Kwenye mitandao ya kijamii Babu Tale anakashifiwa akiitwa mnafiki kutokana na kufahamu suala la Diamond kuzaa na Hamisa na kumficha Zari, hadi pale Diamond alipoliweka jambo hilo hadharani.
Kuhusu hilo, Babu Tale, alisema: “Huwezi kuamini, nimelipenda sana hilo la mimi kuitwa mnafiki. Watu wajue unafiki ndio umenifikisha hapa na umewasaidia wengi kufika mbali, hivyo kashfa za mitandaoni huwa sizijali kabisa na wala haziniumi.”