Hat-trick ilimponza Jeremiah Juma?

KAMA kuna kitu kinampa mawazo straika wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma ni kutocheka na nyavu tangu alipofunga hat-trick dhidi ya Namungo FC, Novemba 27, mwaka jana.
Wakati anapiga stori za hapa na pale na Mwanaspoti, Juma alifunguka wakati mgumu anaopitia wa kumiliki mabao matano yanayowakilisha namba tasa isiyogawanyika, huku shauku yake ikiwa ni kuondoa gundu hilo.
Alieleza mipango yake ni kupambana angalau afunge bao la sita litakalofanya mabao yake yagawanyike, anaamini akifanikisha hilo litampa mwanga wa kutimiza ndoto za kumaliza na mabao 10 msimu huu.
“Katika maisha yangu nachukia kumiliki idadi ya mabao ya namba isiyogawanyika kama tano, sababu inayoninyima usingizi ya kupambania bao la sita ili linirejeshe mchezoni na nisiwe shuhuda wa kuangalia wenzangu wanavyocheka na nyavu,” alisema Juma.
“Uwepo wa wachezaji wageni nafasi ya mbele umechangia kukosa mwendelezo wa kufunga, tulikuwa hatujazoeana namna ya kulishana mipira ya mwisho, maana nilioanza nao kama Salum Kimenya alikuwa majeruhi ila sasa kapona, hivyo naamini tutakaa kwenye mstari.”
Kuna wakati mawazo mabaya yanamjaa Juma, kuona huenda hat-trick imemtia gundu la kuganda na mabao matano, wakati wenzake wanatupia mara kwa mara.
“Tukishinda mechi tatu tutarejea mchezoni, ila hadi sasa naona aliye na nafasi ya kuchukua kiatu cha dhahabu ni Fiston Mayele wa Yanga, ana wachezaji wazuri wanaomzunguka, tofauti na Reliants Lusajo ambaye anatumia nguvu kubwa kupambana mwenyewe,” alisema.
Nje na Juma hakuna mchezaji mwingine anayemiliki hat-trick Ligi Kuu Bara ilipofikia msimu huu.