Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hasira za K’Ogalo kwa Vihiga Bullets

Hasira za K’Ogalo kwa Vihiga Bullets

GOR Mahia wanashuka dimbani leo kuwakabili Vihiga Bullets katika mwendelezo wa mechi za Ligi Kuu Kenya baada ya kutolewa kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

K’Ogalo walipoteza nafasi ya kutinga hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika pale waliposhindwa kutamba mbele ya Otoho d’Oyo ya Congo Brazzaville kwa kukubali kichapo cha jumla ya mabao 2-1 mwishoni mwa wiki iliyopita.

Kocha wa K’Ogalo, Mark Harrison, amesema baada ya kubanduliwa kwenye Kombe la Shirikisho Afrika, lengo lao kuu kwasasa ni kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya waliyoupoteza kwa Tusker FC msimu uliopita.

“Lazima tushinde ligi, tunao mechi Alhamisi (leo) hivyo tusahau ya Otoho d’Oyo na kuzisaka pointi tatu,” alisema kocha huyo raia wa Scotland ambaye pia ashawahi kukipiga katika klabu ya Southampton inayoshiriki Ligi Kuu England.

Gor Mahia wamepania kuendeleza kutofungwa katika mechi za ligi ukizingatia hadi sasa wamecheza mechi sita wakishinda nne na kutoa sare mbili.

Wapinzani wao katika mechi ya leo, Vihiga Bullets, waliopanda daraja, hawajakuwa na mwanzo mzuri wa msimu wakiendelea kusaka ushindi wao wa kwanza. Katika mechi saba walizocheza, Vihiga Bullets wametoa sare moja na kupoteza sita.

Vihiga Bullets watakuwa wakishuka dimbani baada kupoteza mchezo wao wa mwisho dhidi ya KCB kwa mabao 3-1.

Mechi nyingine leo inahusisha AFC Leopards watakao kuwa nyumbani kuwakaribisha Posta Rangers. Mwishoni mwa wikendi iliyopita, Ingwe walipoteza mchezo wao wa tano mfululizo walipofungwa na Bidco United bao 1-0.

Kocha wa Ingwe, Patrick Aussems, anayehusishwa na vilabu vya Azam FC na Namungo zote za Tanzania, anamatumaini hii ndiyo mechi ambayo vijana wake wanaanza safari ya kujikwamua kutoka nafasi za mwishoni mwa msimamo na kusaka nafasi za juu.

Katika Uwanja wa Mbaraki jijini Mombasa, watoto wa nyumbani, Bandari FC, wanawakaribisha KCB ambayo imeshinda mechi zake nne za mwisho.

Hii itakuwa mechi ya tano msimu huu Bandari FC wanacheza mbele ya mashabiki wao wakiwa wameshinda mechi tatu na kupoteza moja. Nao Talanta FC ya Ken Kenyatta ambao hawaonyeshi ugeni wa ligi, watawakabili Bidco United iliyo kwenye morali ya juu hususan baada ya kuwafunga mabingwa wa zamani, AFC Leopards, licha ya kucheza pungufu.

Imeandikwa na ISIJI DOMINIC