Hali ya hewa yazidi kutibuka FKF

Hali ya hewa yazidi kutibuka FKF

Sintofahamu inayoendelea kuikumba uongozi wa soka la Kenya sasa imezua hofu kuhusiana na ikiwa bingwa wa Ligi Kuu ya FKF-PL msimu huu, atapokea pesa zozote za ushindi.

Baada ya Kamati Shikilizi ya FKF kumaliza muhula wake, Waziri wa Michezo aliunda Kamati ya mpito inayoongoza soka kwa sasa. Asilimia kubwa ya wanachama wa Kamati ya Mpito ni wale aliohudumu kwenye kamati Shikilizi kwa miezi sita.

Kamati ya mpito tayari imeiteremsha daraja mabingwa wa Ligi Kuu 2008, Mathare United baada ya kususia mechi tatu mfululizo huku nayo klabu hiyo ikiishtumu kwa kukosa kuwafadhili. Mathare imesema haitokubali uamuzi huo ikisisitiza kuwa Kamati hiyo haina mamlaka ya kuwashusha daraja.

Lakini pia Mathare imeilaumu kamati hiyo kwa kutoipa Sh900,000 kwa wakati kama ilivyoahidi ili kuisaidia kushiriki mechi hizo ilizosusia.

Mtafaruku huu ukiongeza na malalamishi wa marefa hasa wanaochezesha ligi ya divisheni uya pili Nation Super League kukosa kulipwa mishahara yao, imezua tumbo joto kuhusiana na ikiwa bingwa wa ligi kuu msimu huu, atalipwa chochote.

Kidesturi bingwa amekuwa akituzwa kitita cha Sh4 milioni, kiwango kilichoongezwa mwaka jana na afisi iliyokuwepo mabingwa watetezi Tusker FC walipochotewa Sh5 milioni. Lakini sasa, uhakika wa bingwa kuzawadia na pesa kando na kombe msimu huu, haupo tena na hii itategemea mambo kadhaa wa kadhaa.

Mwanchama wa Kamati ya Mpito Ali Amour, anakiri kwamba, uhakika wa bingwa kuzawadiwa na kombe lipo. Hata hivyo kwenye suala la fedha anasema hana uhakika sababu hilo ni suala la kuamuliwa na Wizara ya fedha na kwamba jukumu lao ni kuhakikisha wameiongoza ligi hadi ifike kikomo.

Kamati hiyo ya mpito imeteuliwa kuendesha soka kwa wiki tano pekee. Ligi Kuu imesalia na mechi nnne tu ifike mwisho ikiratibiwa kumalizika Juni 11.

Na huku bingwa akikosa fursa ya kushiriki dimba la CAF Champions League na CAF Confederation Cup, sasa matumaini yapo kwenye kombe na pesa.

“Tulikuwa na lengo la kumtuza bingwa wa Ligi ya FK-PL kombe na fedha. Tayari tumetayarisha bajeti kwa ajili ya utaratibu huo ila sina uhakika kama tutakuwa na mamlaka hayo ya kutuza fedha hizo kwa sababu sisi ni kamati ya muda tu.

Jukumu letu la msingi ni kuhakikisha ligi inafika mwisho salama. Hayo mengine tutayajua baada ya mashauriano na Wizara.”anasema Amour.

Hata hivyo Amour anasema kwenye ripoti waliyomkabidhi Waziri Amina Mohammed baada ya muhula wa Kamati Shikilizi kumalizika, walipendekeza nyongeza ya mtonyo kwa bingwa lakini pia walipendekeza kwamba kila klabu inayosalia kwenye Ligi Kuu ipokee an angalau posho kiasi kwa kutegemea na nafasi watakayomaliza kwenye ligi.