Fei Toto nje wiki mbili

KIUNGO fundi wa mpira wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei Toto’ hatakuwepo kwenye mchezo dhidi ya Azam FC utakaopigwa Aprili 6, kutokana na kupata majeraha akiwa kwenye kambi ya timu ya taifa ‘Taifa Stars’.
Fei aliumia goti na kushindwa kuendelea kufanya mazoezi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Sudan utakaochezwa jioni ya leo kwenye Uwanja wa Mkapa.
Baada ya kupata majeraha hayo alifanyiwa vipimo vya kina na kubainika tatizo lake litamweka nje ya uwanja kwa muda usiopungua wiki mbili na alipewa ruhusa ya kutoka kambini kwenda nyumbani kwao Zanzibar.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fei alisema baada ya kucheza mechi na Afrika ya Kati alimaliza vizuri ila waliporejea mazoezini akiwa anaendelea na ratiba ya programu waliyopewa ndio alipata shida hiyo itakayomuweka nje.
“Nitakuwa nje ya uwanja kwa muda usiopungua wiki mbili baada ya kupata maumivu ya goti, nipo nyumbani Zanzibar naendelea na matibabu, naamini baada ya muda huo nitakuwa sawa,” alisema Fei aliyeifungia Yanga mabao manne hadi sasa kwenye Ligi Kuu Bara.
Kutokana na kuwa nje ya uwanja kwa muda huo, Fei Toto hatakuwa sehemu ya kikosi kitakachocheza mechi ngumu ya ligi dhidi ya Azam na atarejea wakiwa katika maandalizi ya mechi dhidi ya watani wao Simba.
Kukosekana kwa Fei katika mchezo huo dhidi ya Azam kunatoa nafasi kubwa ya kuanza kwa kiungo, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ aliyesajiliwa Yanga akitokea Azam.
Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen alisema Fei aliumia katika mazoezi na kushindwa kuendelea na baada ya vipimo na uangalizi zaidi ilibainika anatakiwa kupata muda wa kupumzika.
Kim alisema muda atakaokuwa nje ya uwanja bila ya kufanya mazoezi au kucheza mechi utakuwa ni wiki mbili ambazo atapaswa kuzitumia kupumzika na kufanya matibabu zaidi kwa ajili ya kurudisha afya yake.
“Fei Toto aliumia goti akiwa hapa Stars, ila baada ya uchunguzi na matibabu zaidi tulikuja kufahamu alikuwa ametonesha maumivu yake aliyokuwa nayo awali kabla ya kujiunga na timu,” alisema Kim na kuongeza;
“Kama unakumbuka wiki kadhaa nyuma Fei akiwa na Yanga kuna nyakati hakuwa sehemu ya timu kutokana na kuumwa goti sasa yale maumivu ndio ametonesha tena na atakuwa nje wiki mbili.”