Dijei Waletee

YAMESEMWA mengi sana. Lakini kuna kitu kimoja tu kinasubiriwa Tanzania nzima. Dijei kuzima muziki na kuwaleta uwanjani Yanga na Simba leo saa 1 usiku. Makocha wamesema kila kitu kiko freshi na mpira utapigwa tena wa kiwango cha juu.

Kocha wa Simba, Zoran Maki na Nasreddine Nabi wa Yanga kila mmoja amechambua dabi hiyo kiufundi huku akiipa nafasi timu yake kushinda na akiwahakikishia pia mashabiki kuja uwanjani kwa wingi na mbwembwe zote kwani lazima mtu apigwe mapema kwa namna yoyote ile.

Zoran amesisitiza kwamba wataendelea walikoishia kwenye raha za Simba Day lakini Nabi akasema kwamba amezungumza na mastaa wake wanajua nini cha kufanya ndani ya dakika 90 kurejesha raha za mashabiki wao. Mechi ya usiku wa leo itatoa jibu la tambo nyingi za sajili za gharama zilizofanywa na timu hizo.

Yanga nyota wapya ambao wanasubiriwa kwa hamu ni Joyce Lomalisa, Aziz Ki Stephane, Lazarous Kambole, Bernard Morrison na Gael Bigirimana. Simba wana Habib Kyombo, Augustine Okrah, Nelson Okwa, Mohamed Ouattara, Dejan Georgjevic, Nassor Kapama na Moses Phiri.


Mechi ya kujilipua

Uwepo wa kundi kubwa la wachezaji ambao kiasili wana tabia ya kupenda kushambulia katika vikosi vya timu hizo, hapana shaka utafanya mechi ya leo iwe ya kushambuliana katika muda mrefu. Mfumo wa 4-2-3-1 una nafasi kubwa ya kutumiwa na kila upande leo ama ule wa 4-3-3 ingawa Yanga wanaweza kutumia ule wa 4-4-2 kutokana na hazina ya kutosha ya washambuliaji wa kati ambao inao kikosini.


Mwamuzi Sasii

Mwamuzi wa kimataifa wa Tanzania, Hery Sasii ndiye amepangwa kuchezesha mechi hiyo ya leo akisaidiwa na Mohamed Mkono na Kassim Mpanga wakati refa wa akiba akiwa ni Ramadhan Kayoko.

Historia inaonyesha mechi zote za Yanga na Simba ambazo refa Sasii amewahi kuchezesha zilimalizika kwa matokeo ya sare katika dakika 90 za mchezo ambapo kabla ya kesho Jumamosi, alishachezesha mechi tatu baina ya timu hizo.

Mchezo wake wa kwanza ulikuwa ni wa Ngao ya Jamii uliochezwa Agosti 2017 ambao uliisha kwa sare bila kufungana na Simba ikaibuka na ushindi wa penalti 5-4 na mechi ya pili ikiwa ni ya Ligi Kuu, Oktoba 2017 ambayo ilimalizika kwa sare ya bao 1-1.

Ukiondoa mechi hizo, Sasii pia alichezesha mechi ya mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu msimu uliopita, Disemba 2021 ambayo ilimalizika kwa sare tasa.


Namba zaibeba Yanga

Kumbukumbu ya mechi 10 za mwisho baina ya timu hizo katika mashindano tofauti zinaonyesha Yanga wamekuwa wababe mbele ya Simba na hilo linaweza kuwaweka katika hali nzuri kisaikolojia katika mchezo huo.

Katika mechi hizo, Yanga imeibuka na ushindi mara tano, Simba imepata ushindi mara mbili na timu hizo zimetoka sare mara tatu.

Hata hivyo, kwenye mechi hizo za Ngao ya Jamii, hili likiwa pambano la 18 tangu ilipoanza kuchezwa mwaka 2001, Simba ndio baba lao kwa kutwaa mara tisa katika misimu 17 ya awali. Simba kama ilivyo Yanga imecheza jumla ya mechi 12 tangu mwaka huo, huku zenyewe kwa zenyewe zimekutana mara saba, huku Simba ikitakata mara nne na Yanga ikishinda mara tatu ikiwamo ya msimu uliopita kwa bao la Fiston Mayele.

Kama Yanga leo itaendeleza ubabe itafikia idadi iliyonayo Simba, lakini pia itaongeza taji la saba kwani kwa sasa ina sita katika mechi zao 12 za awali na ikipoteza sita, tofauti na Simba iliyopoteza mara tatu.


Vikosi vya moto

Wenyeji wa mechi, Yanga huenda kikosi chao kikaundwa na Djigui Diarra, Djuma Shaban, Joyce Lomalisa, Yannick Bangala, Dickson Job, Khalid Aucho, Aziz Ki, Salum Abubakar, Fiston Mayele, Feisal Salum na Farid Musa.

Upande wa Simba kinaweza kuwa na Beno Kakolanya, Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Mohamed Ouattara, Enock Inonga, Jonas Mkude, Pape Sakho, Augustine Okrah, Habib Kyombo, Clatous Chama na Nelson Okwa.

Hata hivyo vikosi hivyo vinaweza kubadilika kutegemeana na uamuzi wa makocha wa timu hizo mbili.


Tiketi nafuu

Kiingilio cha juu cha mchezo huo kwa shabiki atakayeketi katika jukwaa la VIP A ni Sh30,000, wakati VIP ni Sh20,000 na tiketi kwa kiti cha jukwaa la VIP C ni Sh15,000. Viti vya rangi ya machungwa gharama ya tiketi moja ni Sh7000 wakati vile vya kijani gharama ya tiketi ni Sh5,000.