Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dakika 90 za akili nyingi FC Platinum vs Simba

NDANI ya uwanja Simba inajivunia mambo mawili. Asilimia kubwa ya mastaa wenye uzoefu na mashindano ya Afrika pamoja na timu yenye mazoezi, wako fiti kutokana na kucheza Ligi Kuu Bara inayoendelea.

Lakini wenzao wa Platinum wanaocheza nao leo saa 10 jioni mjini Harare, Zimbabwe hawapo fiti sana kutokana na kukosa mechi nyingi za kujiweka sawa kwa kuwa mambo mengi nchini kwao yamesimama kutokana na corona.

Lakini, wanajivunia uzoefu wa wachezaji walioupata kwa kucheza michuano hiyo ya Afrika hatua ya makundi mara mbili mfululizo misimu miwili iliyopita.

Wadadisi wengi wa masuala ya soka wameonya mechi ya leo ni ya akili nyingi na atakayechanga karata vizuri ndiye atakayemaliza mchezo huku faida kubwa ikielekezwa kwa Simba ambao kwenye marudiano Dar es Salaam watakuwa na mashabiki 40,000 jukwaani.

Leo, Platinum hawataruhusiwa kuingiza mashabiki kutokana na corona kama ilivyokuwa kwenye mechi iliyopita dhidi ya Costa do Sol ya Msumbiji. Kama Simba ikiwatoa Platinum mechi ya kwanza ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika itacheza Februari 13, mwakani.

Na kitendo cha Simba kufuzu hatua ya makundi wakiifunga Platinum mechi mbili, watakuwa na uhakika wa Sh1.2 bilioni.

Staa wa zamani wa Yanga, Thabaan Kamusoko amewaambia Platinum FC kwamba Simba sio timu ya mchezomchezo na wanapaswa kutumia akili za ziada kucheza nao kwa kuanzia mchezo wa leo nyumbani.

Kamusoko ambaye Yanga wanamuita ‘kampa kampa tena’, amewatisha Platinum kuwa wakitoka kwenye staili ya uchezaji na kupaniki, Simba ya kina Luis Jose itamaliza mechi leo.

Mzimbabwe huyo ambaye kwa sasa anakipiga Zesco ya Zambia, alisema Platinum ina ubora wa kuiondoa Simba kutokana na rekodi zao kwenye mashindano hayo, lakini akawaambia kuwa Simba ni timu inayotumia nguvu na akili.

Mara ya mwisho kuja Tanzania kimataifa, Platinum ilicheza na Yanga na kutolewa kwa idadi ya mabao 5-2.

“Simba ni timu nzuri na kiukweli Platinum wategemee mchezo wa nguvu sana. Simba imeimarika kwenye miaka ya karibuni, lakini kama Platinum wanaweza kutulia uwezekano wa kuitoa Simba upo.

“Wakienda uwanjani wanapaswa kucheza aina yao ya mchezo na kumheshimu mpinzani, Platinum wakicheza mchezo wao wa kawaida siku zote wana uwezo wa kushinda nyumbani na ugenini,” anasema Kamusoko ambaye alicheza Yanga miaka minne. “Simba ni wazuri sana kwenye kujilinda. Siyo rahisi kuwavuruga na kuwafunga, lakini ukiwapiga presha unaweza kuwafunga kirahisi.

“Simba wana mabeki wazuri, lakini Platinum wakiwa na mpira ni wazuri zaidi, staili yao ya mpira wa kasi.”

Habari zinasema Kocha wa Platinum, Norman Mapeza amepitia video za Simba dhidi ya Plateau kwenye mchezo uliopigwa dimba la Mkapa ili kujua staili na namna ya kuwakabili mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara.

Katika mchezo uliomalizika kwa suluhu na Simba kufuzu ilicheza kwa tahadhari kubwa ikiwemo kujilinda kwa umakini pamoja na kushambulia kwa mipango kupitia pembeni.

Luis ni miongoni mwa mastaa wa Simba waliong’ara kwenye mechi hiyo pamoja na ile ya awali, jambo ambalo linawafanya Platinum wakaze zaidi kupambana naye asiwatie njaa.

Mchezaji wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema endapo kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck akimtumia ipasavyo Luis kwa kumuacha achezee mipira eneo la mbele kuliko kucheza uwanja mzima anaamini mechi ya leo watapata matokeo kupitia faulo au penalti atakazosababisha staa huyo.

Alisema purukushani za Luis na Clatous Chama wakianzia eneo la kati kwenda kufunga zitawasaidia Simba kupata penalti na mipira ya faulo inayoweza kuzalisha mabao na wakaendelea kusonga mbele kwenye michuano hiyo, akisisitiza wanacheza kwa maarifa makubwa.

“Luis ni mchezaji mzuri sana, anaweza akafanya kila kitu, ninachoshauri kama kocha wake ataona ni vyema kukifanyia kazi awe anampa majukumu ya kuchezea mipira eneo la mbele, ufundi wake utawapa presha mabeki, wakitaka kumkaba wanaweza wakasababisha penalti ambazo zitazaa mabao,” alisema Mayay ambaye ni mchambuzi wa soka.

“Kadri Ligi ya Mabingwa inavyocheza ndivyo inakuwa ngumu, hivyo Simba inatakiwa kujisahihisha makosa waliyoyafanya dhidi ya Plateau United licha ya kuingia raundi ya pili, lakini walijikuta wapo kwenye wakati mgumu zaidi.”

Kwa upande wa straika wa zamani wa Simba, Zamoyoni Mogella alisema kwa ukubwa wa michuano hiyo, kocha Sven anatakiwa kuwapanga wachezaji wenye purukushani na mabeki kama Luis na straika Meddie Kagere anayetumia nguvu na hajali kupiga mipira ya vichwa hata kama mabeki wanakwenda kumkaba. “Bocco na Kagere wanatumia nguvu kubwa, lakini maarifa ya kufunga sio mengi, mfano zamani wakati nacheza Stars, Peter Tino - mchezaji wa zamani wa Yanga alikuwa anatafuta mipira kwa nguvu mimi namalizia kufunga au Simba kulikuwa na bonge la baba Zuber Magoha (marehemu) yeye anapambana mimi nafunga, kazi ilikuwa rahisi na tulijua tufanye nini kwenye mechi ngumu,” alisema.

Alimkumbuka Emmanuel Okwi kwamba mechi kama hizi alikuwa anatumia akili kubwa na sio nguvu na kwamba bado pengo lake halijazibika Simba, akishauri wasajili mtu wa aina yake.

Kwa upande wa Amri Kiemba aliyezichezea Simba, Yanga na Azam kwa nyakati tofauti, alisema Wanamsimbazi wana wachezaji wazuri ambao wanaweza wakashangaza kwenye michuano hiyo ni suala la kocha kujua jinsi gani wanaweza wakaleta faida.

“Kuna wachezaji wengi ambao wanaweza wakawa wanacheza kwa akili kubwa kwenye michuano hiyo, kocha awaamini na kuwapa nafasi, mfano kama Kagere ni straika mwenye nguvu ya kupambana na mabeki akipata walishaji wazuri wa mipira ya mwisho,” alisema.


MAGULI ATAWEZA?

Mtanzania Elias Maguli, straika anayetegemewa kwenye kikosi cha kwanza cha FC Platinum alisema kikosi chao ni kizuri licha ya kwamba hawakuwa na ligi, hivyo Simba ijipange kucheza kwa kutumia akili kwani wanataka kufuzu kwa kushinda nyumbani na ugenini.

“Kwanza tumeshinda mechi zote, hii imetujengea kujiamini hivyo Simba inatakiwa kupambana kwa kadri itakavyoweza, wakiongeza bidii na kujitolea zaidi naamini wanaweza wakafanya vizuri na kuipeperusha vyema bendera ya Tanzania, maana zinazokutana ni nchi kwa nchi,” alisema mchezaji huyo na kusisitiza kwamba watacheza kwa kushambulia na suala la kukosa mashabiki haliwezi kuwaathiri.

Kocha wa Simba, Sven Vandenbroeck anasema: “Itakuwa mechi ngumu mno kulingana na FC Platinum walivyo lakini itakuwa mechi yenye mbinu nyingi ndani yake na ushindani wa nguvu hilo tumeliona na tumelifanyia kazi.”

“Unajua katika mashindano haya kadri ambavyo unakwenda katika hatua inayofuata ndio ugumu unaongezeka, ila tutacheza kwa malengo ya kupata matokeo yenye faida kwetu ili tukija katika mechi ya marudiano tusiwe na presha kubwa ya kucheza,” alisema Sven ambaye timu yake ilifika hatua hiyo kwa kushinda bao 1-0 ugenini kwa Plateau United ya Nigeria na kusuluhu dimba la Mkapa.