Chama la Chikwende lapigika

MWENYEJI wa michuano ya Chan mwaka huu nchi ya Cameroon imeanza vyema mashindano hayo kwa kuifunga timu ya taifa ya Zimbabwe bao 1-0 kwenye mchezo wa ufunguzi uliopigwa kwenye dimba la Ahmadou Ahidjo lililopo mjini Yaounde nchini humo.

Zimbabwe ikiwa ni timu ya taifa ya Nyota mpya wa Simba Perfect Chikwende ambaye kwa kiasi kikubwa aliisaidia kufuzu Chan ilionekana kucheza vizuri kwenye kipindi cha kwanza kabla ya kuruhusu bao dakika ya 72 bao lilofungwa na Solomon Banga wa Cameroon na kuwa bao la kwanza katika michuano hiyo mwaka huu.

Ushindi huo uliwapaisha moja kwa moja Cameroon kwenye msimamo wa kundi A na kumshusha Zimbabwe mkiani mwa kundi hilo lenye timu nne na matokeo ya mchezo uliofuata kati ya Mali na Burkina Faso haukubadili nafasi hizo kwakuwa Mali alishinda bao 1-0 hivyo kukaa nafasi ya pili, Burkina Faso wakikaa nafasi ya tatu huku Zimbabwe wakiburuza mkia kwenye kundi hilo baada ya michezo ya kwanza kumalizika.

Baada ya mechi ya Cameroon na Zimbabwe kumalizika, kocha mkuu wa Zimbabwe Zdravko Logarusic alisema vijana wake walionesha kiwango safi lakini matukio ya kishirikina yaliyojitokeza uwanjani yaliwatoa mchezoni.

“Mechi ilikua nzuri, vijana wameweza kupambana lakini matukio ya kishirikina yaliyofanywa na wacameroon kabla ya mchezo ikiwemo kuweka mzoga wa popo katikati ya kiwanja viliwatoa mchezoni,” alisema Logarusic ambaye msimu wa 2013-14 alikuwa akiinoa Simba SC ya Tanzania.

Mechi za kundi B ziliendelea kuchezwa jana huku Dr Congo ikimchapa bao 1-0 Congo na Libya wakitoka sare ya 0-0 dhidi ya Niger.

Mechi za leo Januari 18 ni kundi C itazikutanisha Morocco dhidi ya Togo saa 1:00 usiku huku Rwanda watavaana na Uganda saa 4 usiku.

Tanzania itatupa karata yake ya kwanza kesho dhidi ya Zambia saa 1:00 usiku mechi ya kundi D