Chama katikati ya mtego wa Okwi

Tuesday January 18 2022
Simba kuj PIC
By Olipa Assa

WAKATI mashabiki wa Simba wakichekelea kurejea kwa kiungo Mzambia Clatous Chama, staa huyo ameingia katikati ya mtego wa aliyekuwa mfalme wa kikosi hicho, Emmanuel Okwi aliyewahi kurejea mara tatu na kufanya makubwa Msimbazi.

Chama amerejea kwa mara nyingine ndani ya kikosi hicho, baada ya Simba kumuuza mwaka jana katika klabu ya RS Berkane ya Morocco, kitu kinachoonyesha anapita kwenye nyayo za Okwi, lakini mashabiki wakitaka kumuona amerudi na moto wa aina gani.

Okwi alikuwa kipenzi cha Wanasimba kwa nyakati tofauti alizocheza ndani ya kikosi hicho, alitumika kama kivuli cha viongozi kuwapooza mashabiki wao pindi timu ilipokuwa ikifanya vibaya wanaahidi kumrejesha staa huyo.

Okwi alijiunga kwa mara ya kwanza Simba, 2010-13 na aliyekuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Hassan Dalali alisema kipindi hicho staa alikuwa na umri mdogo, ila mwenye kipaji kikubwa, kilichosuuza mioyo ya mashabiki wa klabu hiyo.

“Tulimsajili kutoka SC Villa ya Uganda, akaondoka 2013 kwenda Étoile du Sahel ya Tunisia mwaka huohuo akarejea Villa, kisha akajiunga na Yanga 2013-2014,” alisema Dalali na kuongeza;

“Okwi anaipenda Simba, akarudi nyumbani 2014/15 akiwa kwenye kiwango kizuri na akauzwa 2015–2017 Sønderjyske ya Denmark na 2017 akarudi tena Villa, kisha akaja Simba na kukaa kutoka 2017 hadi 2019.”

Advertisement

Awamu ya mwisho aliyorejea Simba, ndio aliyofunga mabao mengi zaidi, alitupia 20 katika Ligi Kuu na kuwa Mfungaji Bora kisha akatimkia zake Al Ittihad ya Misri.

Hivyo kurejea kwa Chama kunawapa imani mashabiki, kuona makubwa zaidi kwenye mguu wake kama ilivyokuwa kwa Okwi kila alipokuwa anarejea kiwango chake kiliwafurahisha zaidi mashabiki.

Chama alitwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Bara 2019-2020 na Agosti 7 mwaka jana aliondoka Simba kwenda Rs Berkane akiwa amefunga mabao nane na asisti 13, jambo linalowapa kicheko mashabiki kutegemea kuona makubwa zaidi.

Staa wa zamani wa Simba, Emmanuel Gabriel alisema anatarajia kumuona Chama kama ni Okwi wa pili namna alivyokuwa.

Advertisement