Chama apewa kazi mpya Simba

SIMBA msimu huu imekosa penalti tano na hiyo ni kwenye Ligi Kuu Bara tu weka mbali mashindano mengine.
Lakini, kocha Pablo Franco ameliambia Mwanaspoti kwamba amepata ufumbuzi.
Jukumu hilo la kupiga penalti kama staa wao Clatous Chama atakuwa uwanjani basi atakuwa anasimamia shoo.
Franco alisema Chama atakuwa akichukua jukumu hilo kama chaguo la kwanza kutokana kuwa ndiye mchezaji ambaye anaonyesha kujiamini kupiga penalti akianza na juzi ambapo alipiga penalti nzuri iliyoipa Simba bao la kutangulia dhidi ya Dodoma Jiji.
“Angalia alivyojiamini (Chama). Nafikiri ni vyema kumpa mtu jukumu hili ambaye anaonyesha kujiamini na kama atakuwepo ndani ya uwanja chaguo la kwanza litakuwa kwake,” alisema Franco ambaye Jumapili timu yake itaikabili Berkane kwenye mechi ya Kombe la Shirikisho.
“Ukiangalia wengi wanaonekana kuogopa, nafikiri inatokana na hii baadhi kuzipoteza karibuni. Penalti ni vile mchezaji anajiamini na huwezi kumlazimisha kama unaona hajiamini,” aliongeza
Wachezaji ambao wameingia katika rekodi ya kupoteza penalti Simba ni nahodha John Bocco, Meddie Kagere, Chris Mugalu, Rally Bwalya na Erasto Nyoni.