Bosi mpya Yanga aanza na Al Hilal

Bosi mpya Yanga aanza na Al Hilal

Summary

  • Wakati wowote kuanzia leo, Yanga chini ya utawala wa injinia Hersi Said utatangaza safu mpya ya viongozi watakaojaza nafasi mbalimbali za sekretarieti, lakini bosi wa idara zote hizo ameshaanza kazi kimyakimya huku mezani akiwa na faili la Wasudan wa Al Hilal.

Dar es Salaam. Wakati wowote kuanzia leo, Yanga chini ya utawala wa injinia Hersi Said utatangaza safu mpya ya viongozi watakaojaza nafasi mbalimbali za sekretarieti, lakini bosi wa idara zote hizo ameshaanza kazi kimyakimya huku mezani akiwa na faili la Wasudan wa Al Hilal.

Yanga inakaribia kumtangaza Andrey Mtine kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa klabu hiyo wakimchomoa kutoka klabu kubwa ya TP Mazembe ya DR Congo, lakini taarifa za uhakika ambazo Mwanaspoti inazo ni kwamba bosi huyo ameanza na Al Hilal.

Mtine ameanza kushusha hesabu zote zitakazoisadia Yanga kuwashangaza matajiri hao wa Sudan, ikiwemno mikakati ya kocha wa timu hiyo Florent Ibenge ambaye ni raia wa DR Congo.

Mtine anamjua vizuri Ibenge tangu akiwa anafanya kazi Congo, lakini msimu uliopita tu kocha huyo aliwafanyia umafia na kuwang’oa Mazembe dhidi ya RS Berkane aliyokuwa anaifundisha na kwenda kutwaa taji la Kombe la Shirikisho Afrika.

Mabosi wa Yanga wameshaanza kuchukua tahadhari zote na hesabu zote kutoka kwa Mtine, ambaye pia ameshaanza kuziangalia mechi zote mbili.

Yanga itaanzia nyumbani dhidi ya Al Hilal, Oktoba 8, kabla ya timu hizo kurudiana baada ya wiki moja nchini Sudan, na mshindi wa jumla atatinga hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

“Tumekuwa tukisikiliza ushauri wake, unajua Mtine anajua soka la Afrika, katika kiwango kikubwa mafanikio ya Mazembe amekuwa ndani yake tena mtu wa pembeni kabisa wa tajiri wa klabu, Moise Katumbi,” alisema mmoja wa mabosi wa juu wa Yanga.

“Anajua kuna makosa gani Mazembe iliyafanya tayari ameshatuambia, lakini na yeye anataka kulipa kisasi mbele ya Ibenge, tunafurahi ametuambia tuna kikosi imara kilichobaki ni mipango tu ya kufanikisha kufuzu.”

Jana, Mwananchi lilimshuhudia Mtine akiwa ndani ya kambi ya Yanga akiishuhudia timu hiyo kwa mara ya kwanza ikicheza mchezo wa kirafiki.

Baada ya mchezo huo, Mtine alisalimiana na wachezaji na makocha wote aliowakuta kuanzia msaidizi wa kwanza, Cedric Kaze, ambaye kwa sasa ndiyo anaongoza mazoezi ya kikosi hicho kutokana na Nesreddine Nabi kurejea kwao kwa ruhusa maalumu.