Bocco hatahati, Nyoni atua Stars
TAIFA Stars inatarajiwa kushuka uwanjani kesho Januari 19, 2020 usiku kuvaana na Zambia, huku nahodha wake, John Bocco akiwa katika hatihati kucheza mchezo huo, lakini beki mkongwe wa timu hiyo Erasto Nyoni na Kocha Msaidizi, Seleman Matola wametinga kwenye kambi ya timu hiyo mjini Limbe.
Stars ipo Cameroon kwa ajili ya fainali za Mataifa ya Arika kwa wanaocheza kwenye ardhi ya nyumbani (Chan), ikipangwa kukata utepe dhidi ya Zambia mechi itakayopigwa kesho saa 1:00 usiku kwenye Uwanja wa Limbe.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Cliford Ndimbo alisema Bocco ana hatihati ya kucheza kwani hajajumuika na wenzake mazoezini na inasubiriwa ripoti ya madaktari wao, huku kambi yao ikizidi kunoga baada ya Nyoni na Matola kuwasili huko kuungana na wenzao.
“Nyoni na Matola wameshaungana na wenzao na timu ipo tayari kwa mchezo wa Jumanne dhidi ya Zambia, ila Bocco kuna hatihati ya kucheza inategemea na hali atakayoendelea kuwa nayo,” alisema Ndimbo.
Stars imepangwa Kundi D na timu za Zambia, Guinea na Namibia na hii ni mara ya pili kwao kushiriki fainali hizo za Chan baada ya mwaka 2009 zilipofanyikia Ivory Coast.