Bocco apewa kibarua kipya Simba

Muktasari:

  • Bocco ni kati ya wachezaji waliyohitimu kozi ya ukocha wa utimamu wa mwili iliyofanyika mwezi uliopita katika Ofisi za Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Karume Dar es Salaam na mara baada ya kurudi kambini, mshambuliaji huyo mkongwe amepewa kazi mpya na makocha, Juma Mgunda na Selemani Matola kwa lengo la kuwaonyeha wenzake kile alichokipata mafunzoni.

LICHA ya kuwa na kazi ya kusaka bao lake la kwanza kwenye Ligi Kuu Bara ili kuendeleza rekodi yake ya kufunga misimu 14 mfululizo, nahodha wa Simba, John Bocco kwa sasa amepewa kibarua kipya kambini ambacho huenda mashabiki wa klabu hiyo hawajawahi kujua kabla.

Bocco ni kati ya wachezaji waliyohitimu kozi ya ukocha wa utimamu wa mwili iliyofanyika mwezi uliopita katika Ofisi za Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Karume Dar es Salaam na mara baada ya kurudi kambini, mshambuliaji huyo mkongwe amepewa kazi mpya na makocha, Juma Mgunda na Selemani Matola kwa lengo la kuwaonyeha wenzake kile alichokipata mafunzoni.

Bocco amekuwa akitengeneza programu za mazoezi ya viungo kutokana na elimu aliyoipata muda mchache uliopita, kisha wachezaji wenzake hufuata kama vile anavyowaelekeza na Mwanaspoti imemshuhudia mara kadhaa kambini straika huyo akisimama kama kocha wa viungo.

Katika kila zoezi ambalo Bocco analitoa mwenyewe amekuwa wa kwanza kuonyesha jinsi ambavyo linatakiwa kufanywa kwa usahihi kisha wachezaji wenzake kufuata nyuma kutokana na maelekezo yake.

Wachezaji wa Simba wamekuwa wakifurahia kutokana na uwezo wa kutoa mazoezi ya viungo na kufanyika kwa ufasaha kama inavyohitajika au walivyofanya baadhi ya makocha wa nafasi hiyo waliopita kama, Adel Zrane, Daniel De Castro na Karim Sbai.

Tangu Simba ilipoachana na kocha wa viungo Sbai hadi sasa haina kocha wa nafasi hiyo, huku Mgunda na Matola wakisimamia shoo pengine ndio maana wamekuwa kuna muda wanampa nafasi Bocco kutokana na elimu aliyoipata.

Katika hatua nyingine kikosi cha Simba kitaondoka nchini alfajiri ya Jumamosi kwa ndege ya kukodi kwenda Angola na msafara wao utakuwa na watu 70, wakiwamo wachezaji, benchi la ufundi, viongozi na makundi mengine.

Baada ya mchezo wa Dodoma Jiji wachezaji walikuwa na mapumziko ya siku moja na Jumanne jioni walifanya mazoezi ya kwanza huku wachezaji wawili, Shomary Kapombe na Peter Banda hawakuwa sehemu ya maandalizi hayo kutokana na majeraha.

Habari nyingine njema katika kikosi cha ni urejeo wa winga, Msenegal Pape Sakho aliyekuwa na matatizo ya kifamilia nchini kwao.

Simba itaivaa De Agosto Jumapili katika kuwania kufuzu makundi CAF.