Bin Kleb: Mbona Yanga ndoo yetu hii

YANGA iko katika vita ngumu ya kusaka ubingwa wake wa kwanza ndani ya miaka minne. Wakati presha iko juu, kwa mara ya kwanza kigogo wao mmoja mzito Abdallah Bin Kleb ameibuka na kufungua mdomo wake akiangazia mbio hizo za ubingwa na kuweka wazi mambo mbalimbali.
Kupitia mahojiano maalum na Mwanaspoti Bin Kleb ambaye ni mmoja wa watu wenye nguvu na wanaoheshimika ndani ya klabu hiyo na hata nje anafafanua mambo mbalimbali ya ndani ya klabu hiyo akisisitiza kwamba anatamani kuona utulivu zaidi katika timu hiyo akianza kwa kueleza mbio za ligi anavyozitazama.
MBIO ZA LIGI KUU
“Mwenendo wa ligi sio mbaya sana nashukuru na nafurahi kuiona klabu yangu ya Yanga ndio vinara tunaongoza ligi mpaka hivi sasa. Uwezo wa timu inazidi kuimarika kadiri ya muda unavyosogea japo kuwa kidogo huku mwisho tulipungua kasi, lakini kwa ujumla tunakwenda sawa. Mabadiliko ya mwalimu (Cedric Kaze) aliyoyaleta, mbinu zake zinaonekana kuibadilisha timu na kutulia na niseme ukweli mabadiliko haya yamekuwa na tija kwenye timu yetu. Timu inacheza kwa kutengeneza nafasi, kumiliki mpira, wachezaji wanajua njia za kutafuta mabao ukiangalia kwenye ulinzi pia nadhani Yanga ni timu ambayo imeruhusu mabao machache mpaka sasa (nyuma ya Simba).
“Ukiangalia timu yetu ni kama tuliamua kuanza upya kutokana na karibu asilimia 80 ya wachezaji waliopo ni wapya na wamekuwa na tija katika kikosi chetu, katika hili napenda niwapongeze uongozi wa Yanga lakini pia zaidi wadhamini wetu GSM. Kwa ujumla wamejitahidi sana katika usajili walioufanya. Naweza kusema zaidi ya asilimia 60 hawakukosea. Nina uzoefu kidogo katika usajili, changamoto zinaweza kuwepo na zipo, lakini ni chache na hapo ndipo ninapoamua kuwapongeza sana.
“Unajua usajili wakati mwingine ni kama kamari unaweza kuwa na imani na mchezaji akiwa na ubora mkubwa huko alikotoka lakini akaja kwako akashindwa kuonyesha kile ulichotarajia lakini hapa Yanga imekuwa tofauti kidogo, changamoto ni chache sana, unajua hata wenzetu takwimu zinaonyesha walikumbana na changamoto nyingi za kutafuta timu bora.
YANGA INA KIKOSI DHAIFU
Baadhi ya mashabiki wa Yanga hawana imani na kikosi chao hivi sasa hasa baada ya kutoa sare tatu mfululizo na wameonekana kuishambulia timu yao kwa maneno, lakini Bin Kleb anatoa mtazamo wake katika hili akionyesha kutofautiana nao akisema: “Kwanza nizungumze mimi sio mtaalam sana wa mpira lakini ni mtu wa mpira, na siku zote hakuna timu inayoweza kucheza mechi zote kwa kiwango cha asilimia 100, pili mimi naona tatizo kubwa lililopo kwa wachezaji wetu sasa hivi asilimia kubwa ya wachezaji wa Yanga sasa ni wageni hawajaozea presha ya timu kubwa kama Yanga na hulka ya mashabiki wake.
“Hizi presha zinachangiwa na sisi wenyewe Wanayanga kuipa presha timu yetu hususan wachezaji wetu,kwanza tunaangalia matokeo ya mpinzani wetu (Simba) unakuta wakishinda hata mechi ambazo sisi Yanga hazituhusu zile za kimataifa na baadaye Yanga tukicheza baada ya wao kushinda kisha ikatokea tukapata hata sare baadhi ya wenzetu wanataka kama kutumia nafasi hiyo kulaumu. Mfano hapa kati wenzetu walicheza kule DR Congo dhidi ya AS Vita wakashinda, siku iliyofuata kama sitakosea tulicheza na Mbeya City na tukapata sare baada ya wao kusawazisha dakika ya mwisho kabisa na nakumbuka hali ya uwanja ilikuwa mbovu.
“Niliifuatilia mechi ile kwa umakini sana nilivutiwa jinsi wachezaji walivyopambana, walipigana kufa au kupona kutafuta ushindi, bahati mbaya pia uamuzi wa waamuzi ukawa sio mzuri kwetu sisi tangu mchezo ulivyoanza, sikuelewa ilikuwa kwa bahati mbaya au? Mwishowe Mbeya wakapata penalti katika dakika za mwisho na wakasawazisha. Pale ndipo ilipoanza presha kwenda kwa wachezaji wetu, sisi mashabiki tukaanza kulaumu wakati timu ilicheza vizuri sana.
“Baada ya hapo tuliporudi kucheza nyumbani na Kagera Sugar, ilionekana wazi wachezaji walikuwa na presha kubwa sana ambayo ilizalishwa katika mechi ile ya Mbeya City na mwisho wakapoteza kujiamini tena, wakaacha kucheza mpira wao waliofundishwa. Presha hii tunaizalisha sisi wenyewe kwenda kwa wachezaji wetu badala ya sisi presha tuipate kutoka nje ya Yanga, bahati mbaya sisi ndio tumekuwa tukizalisha presha hii.
ASHTUKIA UMAARUFU MTANDAONI
“Mimi nadhani wapo watu ambao wanapenda kuwa maarufu kwa haraka, unajua sasa mitandao ya kijamii inachukua nafasi sana. Sifurahishwi na wale ambao kila mchezo ukimalizika wanakuja mbele ya mitandao wakionekana kuhojiwa kila mechi inapokwisha na kuanza kutoa maoni yao. Wakati mwingine unaona kabisa ni kama wanafanya kampeni ya kutaka kujulikana au kuonekana kwa watu. Hawa ndio wanaotuharibia utulivu wa timu. Hawajui kwamba vitu kama vile baadaye wachezaji wanaona na vinawapa wakati mgumu.
“Unakuta inafika sehemu mtu anakuja mbele ya vyombo vya habari eti analia kabisa timu kutoa sare au hata imeshinda kwa bao moja sasa unajiuliza timu imeshinda na inaongoza ligi kinachomliza ni kipi? Vipi timu ingefungwa? Kwa hiyo mimi nadhani hawa watu wa namna hii ndio sumu kwa timu yetu. Kwa sasa ingependeza waache hizi tabia.
“Wanachotakiwa mashabiki ni kukumbuka ambako tumetoka, Yanga baada ya kutetereka kiuchumi timu yetu iliyumba kidogo, lakini sasa Mungu ametusaidia tumepata mdhamini ambaye kwangu mimi naona kama ilikuwa ndoto. Hatukuwahi kufikiri anaweza kuja kujitokeza mtu kama GSM kutukomboa na ndani ya muda mfupi akaamua kutusajilia timu bora ambayo ndani ya msimu mmoja tu imeonyesha kuturejeshea furaha. Sasa kupata sare au kushinda goli moja mtu hataki na analia, watu wanatakiwa kuelewa mambo hayawezi kubadilika yote kwa haraka namna hiyo, hata hawa wenzetu hawakuunda timu ndani ya msimu mmoja, walipepesuka sana bora hata sisi.
LAWAMA KWA VIONGOZI
“Sioni pia sababu ya kuwalaumu sana viongozi wa klabu. Unajua watu wanatakiwa kuelewa uongozi ni wanachama, kila mwanachama anatakiwa kushirikiana na uongozi kuhakikisha timu inafanya vizuri na sio kila wakati tunalaumiana tu, hatuwezi kufika. Yapo maeneo ambayo kama wanachama au mashabiki tunatakiwa kuyatumia vyema kwenda kutoa maoni, tunatakiwa kuonyesha utulivu ili tusije kumfanya mdhamini wetu akakata tamaa akaona kana kwamba hatuthamini anachofanya ndani ya klabu yetu hadi mwisho ajiondoe.”
NAFASI YA UBINGWA YANGA
BinKleb anageukia eneo la ubingwa akidai bado anaona kuna nafasi kubwa ya Yanga kuwa bingwa lakini pia akatoa tahadhari yake katika kutafuta mafanikio hayo: “Nafasi ya Yanga kuwa bingwa ipo tena kubwa tu na hii nafasi hatutakiwi kuichezea, tukifanya makosa ya kuendelea kushambuliana wenyewe wa wenyewe wapinzani wetu wanaweza kutumia nafasi hii kutuchanganya ili sisi tupoteane na wao kujiimarisha na kujikuta tunapoteza uongozi wa ligi. Yanga ina spiriti kubwa ya kuutaka na kuuchukua ubingwa msimu huu na hii ni kwa sababu wana hamu kubwa ya kuchukua mataji.
YANGA INAHUJUMIWA?
Zipo kelele nyingi na mitazamo tofauti kutoka kwa mashabiki wa Yanga wakiona kanakwamba timu yao inahujumiwa katika mechi zao. Hapa Binkleb anafunguka:: “Sina hakika kama kweli tunahujumiwa isipokuwa yapo matukio machache katika eneo la waamuzi ambayo yanawafanya watu kufikiria hivyo. Kuna upungufu wa kibinadamu ila wanaofuatilia ubora wa waamuzi waangalie hili linawaumiza wengi na hawalifurahii hasa ukizingatia timu inapambana uwanjani na kila kitu kinaonekana lakini unakuta Yanga inanyimwa haki yake.”
YACOUBA NA SAIDO
Yanga imekosa huduma ya washambuliaji wao muhimu Yacouba Sogne na Said Ntibazonkiza ‘Saido’ na hapa Bin kleb anaitaja kama sehemu ambayo imewapunguzia nguvu kushinda kirahisi.
”Kukosekana kwao kumepunguza pia kasi na ubora wa wachezaji kama Nchimbi (Ditram) na hata Kaseke (Deus) hawa ni wachezaji ambao walianza kuzoeana vyema na naamini kama watarejea haraka watarudisha kitu kikubwa kwenye timu yetu,” anasema Bin Kleb ambaye anafafanua kuwa vigogo wa Yanga waliitwa na bosi wa GSM, Ghalib Said Mohammed kwa ajili ya kuungana kusaidia kuisapoti timu hiyo.