Beki Yanga amtaja Manji

ALIYEKUWA beki wa Yanga, Oscar Joshua amemkumbuka Yusuf Manji, akitoa sababu kwamba enzi zao walikuwa moto kwa sababu walipata kila kitu kwa wakati kutoka kwa mfadhili huyo ambaye pia alikuwa Mwwenyekiti wa Klabu.
Joshua alijiunga na Yanga mwaka 2010 na kuondoka 2017 alisema wao walichukua ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara tatu mfululizo na Kombe la FA, akilinganisha na sasa ambapo wameukosa mara mbili na huu ulikuwa unaenda wa tatu.
Yanga moto anayoisema Joshua ndiye ile iliyokuwa chini ya kocha Hans Pluijm kabla ya hajapokea mikoba George Lwandamina.
“Yanga ilikuwa mwiba kwa timu pinzani, katika mechi moja tulikuwa na uwezo wa kufunga mabao si chini ya mawili, lakini maisha yanaenda kasi inabidi wapambane kadri wawezavyo,” alisema.
YONDANI, ABDUL
Alisema ndani ya kikosi cha Yanga akitazama mabeki Kelvin Yondani na Juma Abdul anaona wamejitahidi kulinda viwango vyao na kwamba wanastahili kuigwa na damu changa.
“Ndio wachezaji waliobakia ambao nilicheza nao, naona wanapambana, umri wao ni tofauti ukilinganisha na uwezo wao wa uwanjani, chipukizi waone wivu kwa hilo,” alisema Oscar huku akimtaja straika wa Namungo FC, Reliants Lusajo kwamba akifanya bidii atafika mbali.