Bei ya mastaa wa Man Utd baada ya janga la corona

MANCHESTER ENGLAND. MANCHESTER United ni nyumba ya baadhi ya wanasoka ghali duniani.
Na hata baada ya janga la virusi vya corona ambalo limeshusha thamani za wachezaji wengi sokoni, lakini huko Old Trafford mambo bado yapo vizuri kimtindo.
TransferMarkt imetoa orodha ya thamani ya sokoni ya kila mchezaji wa Man United huko Old Trafford, ikizingatia zaidi uwezo wa kila mchezaji, umri, kiwango na historia ya uhamisho.
Kwa mujibu wa tovuti hiyo, thamani ya wachezaji wa Man United sokoni, ambapo mwenye thamani kubwa katika kipindi hiki cha corona ni Pauni 72 milioni, huku kukiwa na zaidi ya wachezaji 10 ambao thamani yao ya sokoni inakaribia Pauni 20 milioni licha ya kuwapo kwa janga la corono lililoshusha uchumi wa dunia.
Hii hapa ndio orodha ya wachezaji wa Man United wenye thamani kubwa sokoni katika kipindi hiki dunia ikiwa imetikiswa uchumi wake kutokana na janga linalosababishwa na COVID-19.
10.Diogo Dalot, Pauni 16.20 milioni
Kwenye namba 10, anashika staa wa Kireno, Diogo Dalot, ambaye alinaswa na Man United kwa ada ya Pauni 19 milioni kipindi timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Jose Mourinho. Kwa mujibu wa TransferMarkt, Dalot kwa sasa thamani yake ni Pauni 16.20 milioni katika kipindi hiki cha corona.
9.Scott McTominay, Pauni 20.25 milioni
Kiungo kinda, McTominay ni moja ya wacheza ambao thamani zao bado zipo juu kimtindo sokoni licha ya kwamba janga la corona. Staa huyo kwa sasa thamani yake sokoni ni Pauni 20.25 milioni. Staa mwingine mwenye thamani kama hiyo ya Pauni 20.25 milioni ni winga, Daniel James, ambaye aliigharimu timu hiyo Pauni 17 milioni aliponaswa mwaka jana.
8.Victor Lindelof, Pauni 25.20 milioni
Man United ilitoa Pauni 31 milioni kunasa huduma ya beki huyo wa kati wa kutoka Sweden. Baada ya kutamba kwa muda kwenye kikosi hicho cha Old Trafford, beki Victor Lindelof, thamani yake ya sasa sokoni ni Pauni 25.20 milioni. Thamani hiyo ni katika kipindi hiki cha corona ambacho kimefanya thamani za wachezaji wengi sana thamani zao kushuka.
7.Mason Greenwood, Pauni 26.10 milioni
Ni mchezaji mwingine aliyeibukia kutoka kwenye akademia ya klabu hiyo ya Old Trafford. Na sasa kinda huyo ukilitaja jina lake ni pesa tu kutokana na thamani yake sokoni kuwa Pauni 26.10 milioni. Greenwood amekuwa akipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho cha Man United kwa sasa ikiwa chini ya kocha Ole Gunnar Solskjaer.
6.Aaron Wan-Bissaka, Pauni 28.80 milioni
Man United imemfanya Wan-Bissaka kuwa mmoja wa mabeki ghali duniani wakati ilipomnasa kwa Pauni 50 milioni kutoka Crystal Palace katika dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana. Lakini, kutokana na janga la corona, Wan-Bissaka thamani yake sokoni imeshuka na imefikia Pauni 28.80 milioni. Beki hiyo wa kulia, raia wa England ni moja ya wachezaji walio kwenye kiwango kikubwa kabisa cha soka kwa sasa.
5.David De Gea, Pauni 36 milioni
Kwa mujibu wa TransferMarkt, thamani ya sasa ya kipa David De Gea huko sokoni ni Pauni 36 milioni, ikidai ni baada ya uchumi kutikiswa ma janga la corona. De Gea, ambaye ni Mhispaniola, amekuwa akitajwa kuwa kipa mahiri duniani kwa sasa. Si muda mrefu uliopita De Gea alikuwa akihesabika kuwa kipa bora kabisa duniani kabla ya kipindi cha karibuni kiwango chake kushuka na kuibuka kwa mjadala kwamba, huenda anahitaji kubadilishwa langoni kwa sasa.
4.Bruno Fernandes, Pauni 43.2 milioni
Man United ilizama mfukoni na kutoa Pauni 47 millioni kunasa huduma ya kiungo wa Kireno, Bruno Fernandes. Tangu atue Old Trafford, Bruno amekuwa moto kwelikweli na kurudisha ari ya kiuchezaji kwenye kikosi hicho. Thamani hiyo sokoni ya Bruno katika kipindi hiki cha corona, inalingana pia na winga wa Kifaransa, Anthony Martial, ambaye pia TransferMarkt inamthaminisha kuwa na thamani ya Pauni 43.2 milioni huko sokoni kwa sasa katika mtikisiko wa uchumi unaotokana na janga la corona.
3.Harry Maguire, Pauni 50.40 milioni
Wakati Man United ilipokwenda Leicester City kwenda kunasa saini ya beki wa kati, Harry Maguire iliwagharimu Pauni 80 milioni. Jambo hilo, linamfanya Maguire kuwa mmoja wa mabeki ghali duniani.
Hata hivyo, janga la corona limemfanya Maguire kushindwa kulinda thamani yake sokoni baada ya sasa, beki huyo wa kati, kuwa na thamani ya Pauni 50.40 milioni kwa mujibu wa TransferMarkt. Maguire ndiye nahodha wa Man United kwa sasa akiaminiwa na kocha Ole Gunnar Solskjaer.
2.Marcus Rashford,
Pauni 57.60 milioni
Wakati wachezaji walionaswa kwa pesa nyingi kama Wan-Bissaka na Maguire thamani zao zikishuka tofauti na pesa zilizotumika kunasa saini zao, zao la kutoka kwenye akademia ya Man United, Marcus Rashford thamani yake imepanda.
Kwa mujibu wa TransferMarkt, thamani ya Rashford sokoni kwa sasa katika kipindi hiki cha coroni ni Pauni 57.60 milioni. Rashford ni moja ya washambuliaji wanaoaminika na kocha wa Man United akiamini ataendelea kufanya mambo makubwa kwenye kikosi chake.
1.Paul Pogba, Pauni 72 milioni
Siku za karibuni kinachosemwa kuhusu Paul Pogba ni kuwa na mpango wa kuhama Man United huku Real Madrid na Juventus zikitajwa kuwinda saini yake. Man United wao walilipa Pauni 89 milioni kumsajili ilipomrudisha Old Trafford kutoka Juventus mwaka 2016. Kwenye dirisha la kiangazi la mwaka jana, Man United ilisema thamani ya mchezaji huyo ni Pauni 150 milioni, kisha ilipandisha hadi Pauni 180 milioni ili kuwazuia Real Madrid wasimchukue.
Lakini baada ya janga la corona, TransferMarkt inamthamini Pogba kuwa na thamani ya Pauni 72 milioni huko sokoni kwa sasa.
Wachezaji wengine
Baada ya kuona ya wachezaji wa Man United wenye thamani kubwa sokoni kwa sasa baada ya janga la virusi vya corona, wachezaji ambao hawajaorodheshwa hapo, thamani zao zipo chini zaidi.
Wachezaji hao kama vile Nemanja Matic, Juan Mata, Jesse Lingard, Fred, Luke Shaw, Sergio Romero, Eric Bailly, Phil Jones, Tuanzebe na wengineo.