Bangala, Aucho wana jambo lao

KOCHA wa Yanga, Nasreddine Nabi amewakabidhi mastaa watano mechi ngumu ya fainali ya FA dhidi ya Coastal Union leo Jijini Arusha.
Nabi ambaye amebeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara, mastaa aliowapa mapumziko na kuwapa pumzi kubwa tayari kwa fainali ni Yanick Bangala, Djugui Diarra, Dickson Job, Khalid Aucho, Abubakar Salum na Djuma Shaban.
Wachezaji hao hakuwachezesha kwenye mechi ya kulinda heshima dhidi ya Mtibwa na akasema kabisa kwamba nguvu yao kubwa anaitaka Arusha kwenye ubingwa.
Alisema Yanga inakwenda kucheza mchezo mgumu dhidi ya Coastal Union katika kipindi cha hivi karibuni timu yao imeimarika tofauti na ilivyokuwa mzunguko wa kwanza haikuwa imara kama wakati huu ambao nao wanataka kwenda kimataifa.
“Mchezo wa fainali utakuwa tofauti na zile mechi mbili katika ligi,mahitaji yalivyo wakati huu tunaenda kucheza na timu ngumu yenye historia ya kupata matokeo mazuri dhidi ya Yanga,” alisema Nabi na kuongeza; “Wapinzani wetu wamemaliza msimu vizuri kwa kiwango bora tofauti na mwanzo wa ligi pamoja na kushinda nusu fainali wakicheza na timu kubwa nchini Azam.
“Malengo yetu ni kushinda mechi hii na kuchukua ubingwa ila tunakwenda kucheza na timu yenye ushindani wa kutosha, tupo katika maandalizi mazuri kulingana na wapinzani walivyo ili kushinda mchezo huo,” alisema Nabi na kuongeza;
“Baada ya mchezo huo kumalizika tutakuwa na ratiba ya mapumziko huku viongozi wakiendelea kusimamia mahala ambapo tutakwenda kwa ajili ya kambi, kukamilisha usajili na mambo ya msingi kwa ajili ya msimu ujao,
“Mafanikio ya msimu huu nitajitahidi kuandaa timu ili kufanya hivyo msimu ujao katika mashindano ya ndani pamoja na yale ya kimataifa tuliyoishia hatua ya awali,”alisema Nabi akikiri kwamba dhidi ya Mtibwa licha ya kushinda walicheza kawaida sana na sicho watakachofanya Arusha.