Banda, Gadiel kimewaka simba

Banda aitanguliza Simba

MASHABIKI wa Simba kwasasa ni furaha tu baada ya kuona kila mchezaji wao anaonyesha kiwango kizuri pale anapopewa nafasi kwenye kikosi chao.

Kocha Mkuu wa timu hiyo, Pablo Franco tangu ajiunge na Simba akioongoza mechi tatu ameonyesha kubadili badili kikosi chake akiwapa nafasi wachezaji wote. Katika mchezo wao na Geita, Pablo alimuanzisha Peter Banda akicheza kwa kiwango kikubwa na kufunga bao moja katika ushindi wa 2-1.

Pia alimpa nafasi beki Gadiel Michael aliyecheza dakika 90 baada ya mchezo wao dhidi ya Ruvu Shooting kumpa dakika tano tu.

Wadau wa soka wamempongeza kocha huyo kutoa nafasi kwa wachezaji hao. Aliyekuwa Meneja wa Biashara United na sasa kocha mkuu wa Korosho FC, Aman Josiah alisema; “Haijalishi hata kama angekuwa amefunga kwa mkwaju wa penalti bado ingekuwa na maana kubwa kwake, kisaikolojia hadi dakika hii amejengeka na ninaamini atakuwa bora zaidi,” alisema Aman na kuongeza:

“Kwa upande wa Gadiel na yeye ni jambo zuri kucheza lakini kwa nafasi yake kama wangeshinda bila kuruhusu bao ndio ingekuwa na maana zaidi, lakini simsemi kwa sababu kuruhusu nyavu zao kuguswa ni ishu ya safu ya ulinzi yote.”

Kipa wa zamani Simba, Idd Pazi alisema Banda na Gadiel walionyesha kiwango kizuri na hilo ni fundisho kubwa kwa makocha wengine kuwapa nafasi wachezaji wao.

“Gadiel ni mchezaji mzuri na alishacheza hadi timu ya Taifa kwenye mashindano makubwa kwahiyo sio kwamba ni mbaya bali tu hapati nafasi ya kucheza kwenye timu, sawa pia na upande wa Banda.

Pablo alisema kila mchezaji atakuwa anapata nafasi ya kucheza kwa sababu akikaa bila kucheza anapoteza hali ya kujiamini ndani ya uwanja.