Bajeti Simba inaposajili Uarabuni

Muktasari:

  • Wanapaswa kufahamu kuwa kwa bajeti ya Sh 6 bilioni, kuingia hatua ya makundi kwao itakuwa ni mafanikio makubwa kuliko kujidanganya kuwa ni miongoni mwa washindani wa ubingwa wakati kuna timu ambazo zinasajili wachezaji watatu tu kwa bajeti ambayo wao wanaitumia msimu mzima.

NOVEMBA nne mwaka huu, Simba ilitangaza bajeti ya Sh 6 bilioni kwa ajili ya matumizi ya shughuli mbalimbali katika msimu wa 2018/2019.

Bajeti ambayo itagharamia uendeshaji wa klabu hiyo ambayo itakabiliwa na Mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu, Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi katika msimu huu ulioanza Agosti mwaka huu.

Kwa wenye kumbukumbu nzuri watakubaliana nami kuwa bajeti hiyo iliyotangazwa kuna ongezeko la takribani Sh 2 bilioni katika kiasi cha Sh 4 bilioni ambacho ndio ilikuwa bajeti ya Simba msimu uliopita.

Kwa kundi kubwa la mashabiki, wapenzi na wanachama wa Simba, wanaiona ni bajeti ya kitemi mno ambayo itaifanya timu yao itikise katika mashindano mbalimbali itakayoshiriki nje na ndani ya nchi.

Ni vigumu kuwaondoa Wanasimba nje ya mawazo hayo. Wengi wao wanaamini kuwa kama timu yao imetenga kiasi kikubwa cha bajeti kuliko nyingine zinazoshiriki kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kuna kikwazo gani cha kuwazuia kwenye mashindano yaliyo mbele yao?

Unadhani wanakosea? Hapana. Fedha ina maana na thamani kubwa kwenye soka, siku kadhaa baada ya mkutano ule uliotangaza bajeti ya Simba, klabu mbili kutoka Kaskazini mwa Bara la Afrika zilikuwa na mechi mbili za kibabe za hatua ya fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Klabu ya Al Ahly ya Misri ambayo ni mabingwa wa kihistoria wa mashindano hayo wakiwa wametwaa taji hilo mara nane, walikuwa na vita mbele ya Waarabu wenzao kutoka Tunisia, Esperance ambao wao wamechukua ubingwa huo mara tatu.

Esperance ilitoka kifua mbele na kutwaa ubingwa kwa ushindi wa jumla wa mabao 4-3 wakianza kwa kufungwa mabao 3-1 ugenini kabla ya kupindua meza nyumbani na kushinda mabao 3-0. Sikushtushwa na matokeo, bali thamani ya usajili wa nyota wanaounda vikosi vya Esperance na Al Ahly ndio lililoniacha nikiwa kwenye mshangao nikilinganisha na hapa nyumbani.

Kwenye kikosi cha kila timu, idadi ya wachezaji watatu tu thamani yao sokoni kwa sasa inafikia bajeti ile iliyotangazwa na Simba kwenye mkutano wao mkuu (Sh 6 bilioni) na pengine inaizidi kabisa. Katika kikosi cha Al Ahly, thamani ya kipa, Mohammed El Shenawy sokoni kwa sasa ni Pauni 1 milioni (Sh 3 bilioni), thamani ya mchezaji, Walid Soliman ni kiasi cha Pauni 600,000 ambazo ni zaidi ya Sh 1.8 bilioni huku staa mwingine wa kikosi hicho, Hossam Ashouri akiwa na thamani ya Pauni 1.2 milioni (zaidi ya Sh 3.6 bilioni).

Hii inamaanisha thamani ya nyota hao watatu tu wa kikosi cha Al Ahly inazidi bajeti iliyotengwa na Simba msimu kwani kwa jumla, wachezaji hao wana thamani ya Sh 7.4 bilioni. Upande wa pili wa Esperance, mastaa wake, Anice Badri, Coulibary pamoja na Saad Bguir thamani yao kwa pamoja ni zaidi ya Sh 9 bilioni za Kitanzania ikiwa ni ongezeko la Sh 3 bilioni kwenye ile bajeti iliyotangazwa kitemi na Simba pale kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Julius Nyerere, Posta Mpya jijini.

Thamani hii ya nyota wachache katika vikosi vya Esperance na Al Ahly inatukumbusha bado tuna safari ndefu na kazi kubwa ya kufanya ili tuweze kufika pale walipo wenzetu.

Inapofikia hatua bajeti ya klabu inayoonekana kuwa ndio kubwa zaidi katika nchi, inazidiwa na thamani ya wachezaji watatu tu wa kikosi cha timu moja kutoka nchi nyingine, inatoa picha ya wazi kuwa kuna uwezekano mdogo kwa timu zetu kufanya vizuri kwenye mashindano ya klabu barani Afrika.

Tuwapongeze Simba kwa kile walichokianza kupitia mfumo mpya wa kampuni katika uendeshaji wa klabu yao lakini hawapaswi kupewa presha na matumaini makubwa ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya Afrika kwa bajeti yao Sh 6 bilioni. Kuna kazi kubwa ipo mbele ya Bodi ya Wakurugenzi wa Simba katika kukuza thamani ya klabu hiyo ili kuhakikisha inakuwa na misuli imara ya kiuchumi siku za usoni ili nayo iwe na uwezo wa kusajili mchezaji kwa thamani hata ya Sh 3 bilioni kama ambavyo Al Ahly na Esperance zinaweza kufanya kwa sasa.

Kuelekea mashindano ya kimataifa, pamoja na bajeti ya Sh 6 bilioni iliyotenga, mashabiki wa Simba wanapaswa kuujua ukweli mchungu kuwa bado thamani na ubora wa kikosi chao sio tishio.