Baada ya kikao... Wachezaji Simba waahidi raha

VIGOGO wa Simba wamekaa kikao cha wazi na wachezaji wao na benchi la ufundi kujadiliana mambo mbalimbali, wameafikiana kwamba kuanzia leo dhidi ya Mwadui mambo yatakwenda sawa.

Viongozi wa mabingwa hao watetezi juzi (Alhamisi) saa 8:00 mchana walikwenda katika kambi ya timu iliyopo Bunju na kufanya kikao na wachezaji na benchi la ufundi ambacho kilikuwa cha maana baada ya kuafikiana mambo mengi.

Kikao hicho kilichochukua si chini ya saa 1:30, viongozi waliongozwa na Ofisa Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez walizungumza na wachezaji pamoja na benchi la ufundi ambalo liliongozwa na kocha mkuu, Sven Vandenbroeck.

Ajenda kubwa ilikuwa ni matokeo mabaya ambayo waliyapata katika michezo miwili iliyopita, mwenendo wa timu, mabadiliko yaliyofanyika ndani ya timu pamoja na masuala mengine binafsi.

Baada ya ajenda hizo zote kuzungumzwa Sven alizungumza kwa niaba ya benchi la ufundi na kueleza mbele ya uongozi mambo yatakuwa mazuri katika michezo ijayo na wachezaji nao kila mmoja alizungumza kwa nafasi yake kuwa walipoteza kwa bahati mbaya na watapambana na kujituma katika michezo ijayo.

Katika kikao hicho Barbara aliungana na baadhi ya wajumbe wa bodi pamoja na Mkuu wa Idara ya Uendeshaji, Arnold Kashembe. Ingawa viongozi wa Simba walikausha kuzungumzia ishu hiyo jana kwa madai kwamba ni mambo yao ya kawaida ya ndani, Luís Miquissone alisema kupoteza katika michezo miwili mfululizo ni jambo ambalo linaweza kutokea katika kikosi chochote hata kama wakiwa na kikosi chenye wachezaji bora zaidi ya waliopo.

Miquissone alisema kufungwa mechi mbili sio mashabiki pekee waliumia, bali wachezaji ilikuwa zaidi kwani wao ndio wanahusika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa wanacheza na wanaendesha maisha kupitia kazi hiyo.

“Presha iliyokuwepo ni baada ya kukosa ushindi kwenye mechi tatu, lakini ndio mchezo wa mpira ulivyo ila mashabiki wetu wasikate tamaa wajitokeze kwa wingi katika mechi inayofuata,” alisema.