Awesu sasa amtaja Maxime Azam FC

Awesu sasa amtaja Maxime Azam FC

KIUNGO fundi wa mpira wa Azam FC, Awesu Awesu amesema kipindi cha Kocha Aristica Cioaba hakuwa na wakati mzuri haswa kusugua benchi hivyo, anajipanga kumshawishi kocha mpya ajaye, huku akimtaja kocha wake wa zamani, Mecky Mexime.

Awesu aliyekuwa na kiwango bora tangu akiwa na kikosi cha Madini FC kabla ya kujiunga na timu za Mwadui na Kagera Sugar, lakini tangu atue Azam amekuwa na wakati mgumu kupata namba.

Katika mechi 13 za timu yake, nyota huyo kutoka Zanzibar amecheza mechi nne huku akianza katika kikosi cha kwanza mchezo mmoja dhidi ya Coastal Union waliposhinda mabao 2-0.

Hata hivyo, tayari Azam imeshamtupia virago kocha Cioaba, huku taarifa zikidai matajiri hao wanamshusha kocha wa zamani wa Yanga na Zesco United, George Lwandamina kukinoa kikosi hicho.

Akizungumza jijini hapa, Awesu alisema hajawa na mwenendo mzuri na hiyo ni kutokana na kutopewa nafasi uwanjani kwani aliyekuwa kocha wao aliwahitaji zaidi, Never Tigere na Salum Aboubakari ‘Sure Boy’.

Alisema kwa sasa anaendelea kujifua huku akiweka matumaini kwa kocha mpya ajaye ili kuweza kumshawishi ili kumuamini na kumpa namba ili kuendeleza kiwango chake.

“Hakuna mchezaji anayependa kukaa benchi, lakini kila Kocha ana falasafa yake, yule aliona mimi siwezi, ila angekuwa ni Mecky Maxime mngeniona Awesu yuleyule,” alisema kiungo huyo mwenye kasi uwanjani.

BY SADDAM SADICK