Vifo hivi vya wachezaji viwaamshe TFF

Marehemu Marc Vivien Foe enzi za uhai wake.
Muktasari:
Foe alifariki duniani katika mechi ya Kombe la Mabara kati ya Cameroon na Colombia baada ya kuanguka ghafla uwanjani katika dakika ya 72.
ASUBUHI ya Juni 27, 2003 habari kubwa iliyokuwa ikizungumzwa na wadau wa soka ni kuhusu kifo cha mwanasoka wa Cameroon, Marc Vivien Foe.
Foe alifariki duniani katika mechi ya Kombe la Mabara kati ya Cameroon na Colombia baada ya kuanguka ghafla uwanjani katika dakika ya 72.
Kifo hicho kiliibua simanzi kwa wadau wa soka huku baadhi yao wakihoji inakuwaje mchezaji wa hadhi ya kimataifa aanguke ghafla uwanjani na kufariki, je, alipimwa kabla ya mechi au hakupimwa?
Wakati kifo cha mchezaji huyo kikianza kusahaulika, Mei 6 mwaka huu, kwa mara nyingine kimetokea kifo cha mchezaji mwingine, Patrick Ekeng ambaye pia ni wa Cameroon.
Ekeng, anayeichezea klabu ya Dinamo Bucharest ya Romania, alifariki dunia katika mechi ya Ngao ya Hisani dhidi ya Viitorul Constanta, mechi ambayo ilimalizika kwa sare ya mabao 3-3.
Siku tatu baada ya kifo cha Ekeng, kipa wa timu ya wanawake ya Femina Stars ya Cameroon, Jeanine Christelle Djomnang alifariki akiwa anapasha viungo moto kabla ya mechi ya ligi dhidi ya Louves Yaounde.
Tunajua kwamba hata hapa Tanzania vimewahi kutokea vifo vya wachezaji uwanjani na zaidi kinachozungumzwa au kilichomo kwenye kumbukumbu za historia kwa wengi ni kifo cha mchezaji wa zamani wa Simba, Hussein Tindwa.
Tindwa alifariki miaka ya 1970 wakati akiiwakilisha Simba katika mechi ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya Raccah Rovers ya Nigeria Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) Dar es Salaam.
Tunatambua imani ya wengi kwamba kufa kupo lakini pia ni vyema kukumbushana umuhimu wa kuchukua tahadhari ili kuepusha si vifo tu, bali hata majanga mengine ya kiafya.
Tunachotaka kusisitiza hapa ni umuhimu wa wachezaji kupimwa afya zao, si tu wakati wa usajili, bali zoezi la upimaji afya za wachezaji liwe endelevu, kabla, baada na ikibidi hata katikati ya msimu.
Tumekuwa tukiripoti matukio ya baadhi ya wachezaji kupimwa afya zao, lakini matukio hayo yamekuwa yakijitokeza pale wachezaji wanaposajiliwa na si kwa wachezaji wote, bali ni baadhi hasa wale wa kigeni. Kwa hali hiyo ni muhimu kwa TFF kuhakikisha wanatafuta utaratibu ambao utawafanya viongozi wa klabu kuwa na utaratibu wa kupima afya za wachezaji wao mara kwa mara.
Utaratibu wa kumsajili mchezaji baada ya kujiridhisha kwamba ana kipaji kwa sasa umepitwa na wakati ni vyema pamoja na kipaji hicho afya ya mchezaji nayo ipewe uzito unaostahili.
Na hapa tungependa kuona mchezaji anafanyiwa vipimo vya afya katika hospitali au vituo vya afya vinavyoeleweka na si vile vya uchochoroni au kama ni mtaalamu, basi awe yule ambaye utaalamu wake hautiliwi shaka, awe amekamilika. Tunalisisitiza jambo hili si kwa sababu ya vifo, bali ni utaratibu wa kawaida wa kuchukua tahadhari katika michezo kama ambavyo imekuwa ikifanyika kwingineko na hivyo si vizuri Tanzania kujitenga katika utaratibu huu.