Kwenye ngumi ni hivi tu

Februari 17, 1999: Evander Holyfield (kulia) akizichapa na Lennox Lewis 

Muktasari:

  • Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha miaka ya nyuma, mambo yalikuwa magumu zaidi kwani mabondia wengi walikimbilia katika ngumi za ridhaa

KUMEKUWAPO na ushindani mkubwa katika mchezo wa ngumi, na hii ni katika miaka ya karibuni, ambapo mabondia wengi wanapambana kuhakikisha kwamba wanapenya katika eneo la ngumi za kulipwa ili wakanufaike na kipato kinachodaiw akuongezeka miaka ya karibuni.

Itakumbukwa kwamba, katika kipindi cha miaka ya nyuma, mambo yalikuwa magumu zaidi kwani mabondia wengi walikimbilia katika ngumi za ridhaa ambako walikita mizizi na miongoni mwao walijipatia umaarufu mkubwa, lakini hata walipotangulia mbele za haki hawakuacha alama inayolingana na umahiri wao ulingoni.

Hata hivyo, kadri miaka ilivyosonga hivi sasa ngumi zinalipa na kila kijana mwenye matamanio ya kuingia katika fani hii amekuwa akifikiria manufaa zaidi kuliko kupigana tu ilimradi awafurahishe watu.

Kwa ujumla michezo yote katika miaka ya karibuni imekuwa ni ajira na ni wazi kwamba mtu anaweza kuingia katika sekta hii na kunufaika nayo. Lakini je kuna mtamanio hilo kwa vijana wasio na ajira?

Katika ngumi, licha ya mapromota tuliozoa kuwaona wakiandaa mapambano makubwa, lakini hivi sasa kuna mapromota wapya wengi wanajitokeza kuwekeza kwenye mchezo huo na kuupa uhai zaidi unaoufanya uwe kimbilio sahihi kwa vijana.

Tunafahamu, ngumi za kulipwa ni biashara. Huu ni ni mchezo wa nipe nikupe kwani bondia anasaini mkataba kabla ya pambano na  akipigwa au kushinda pesa yake iko palepale na kila upande una dau lake kulingana na renki na rekodi za bondia husika.

Hili ndilo jambo muhimu zaidi, japokuwa huwa kuna adhabu ya kutolipwa au kupunguziwa malipo kama bondia ataonekana amepanga matokeo kwa kujiangusha ulingoni, lakini vinginevyo malipo yapo palepale.

Hapa nchini baada ya soka, ngumi hasa za kulipwa huenda ndiyo ukawa mchezo unaofuatia kwa kuwa na mashabiki wengi katika miaka ya karibuni, kwani ile dhana kwamba ngumi ni uhuni sasa imetoweka na mabondia wanauchukulia ni kazi ya kuwaingizia kipato.

Hata mashabiki, sio tena wale wa ilimradi kama ilivyokuwa imezoweleka miaka ya nyuma, ingawa hao nao wapo, lakini pia wanafuatilia kwa kina kuujua mchezo husika na pia takwimu zake. 

Pamoja na hayo, lakini hivi sasa mtu kujifunza ngumi ni rahisi sana kwani yanashuhudiwa mapambano yanachezwa kwenye mazingira rafiki kwa mashabiki wa rika na jinsia zote kufuatilia mchezo hata wakiwa na familia zao ukumbini ama nyumbani tofauti na miaka 15 iliyopita shabiki akienda kwenye ngumi lazima ajiandae kukabiliana na lolote linaloweza kutokea.

Kwa maana nyingine ngumi ni mchezo wa heshima kubwa kwa sasa na hivyo huu ni mchezo sahihi kwa sasa kwa vijana kuukimbilia ili wautumie kama mojawapo wa ajira za kimichezo.