Kipigo cha Toto kiirudishe Simba kwenye mstari

Muktasari:
Mashindano hayo yaliibua matumaini mapya kwa Simba kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani kwa kuwa timu inayobeba Kombe la FA ndiyo inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
SIMBA imetolewa katika mbio za kusaka ubingwa wa Kombe la FA baada ya kushindwa kuchapwa mabao 2-1 na Coastal Union ya Tanga.
Mashindano hayo yaliibua matumaini mapya kwa Simba kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani kwa kuwa timu inayobeba Kombe la FA ndiyo inayoshiriki Kombe la Shirikisho Afrika.
Baada ya kipigo hicho mashabiki wa Simba walijifariji wakiamini kwamba, klabu yao iliteleza na kwamba bado kulikuwa na fursa nyingine ya kufanya vizuri.
Fursa iliyoonekana hapo ni Ligi Kuu Bara ambako Simba ilikuwa ikishika usukani na matarajio ya wengi ni kwamba kasi yao ya ushindi wangeendelea nayo katika ligi hiyo.
Katika hali ambayo haikutarajiwa, timu hiyo ililala kwa bao 1-0 mbele ya Toto Africans ya Mwanza, katika mechi iliyopigwa juzi Jumapili Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Matokeo hayo ambayo hayakutarajiwa yameonekana kufifisha matumaini ya Simba kuiwakilisha Tanzania kwenye michuano ya kimataifa mwakani.
Kwa hali hiyo zile kelele za mahasimu wao Yanga kwamba, Simba ni wa mchangani zitaendelea kusikika siku hadi siku kwa kuwa klabu hiyo sasa ni kama imekwama.
Kibaya zaidi ni kwamba matokeo dhidi ya Toto yameibua sintofahamu baina ya wachezaji wa Simba ambao, wamediriki kupigana mara baada ya mechi hiyo.
Hata hivyo kwa upande wetu tunadhani kilichojitokeza sasa ndani ya Simba ni mfano wa upepo mchafu ambao viongozi wanatakiwa kukabiliana nao kwa nguvu zote.
Kama kuna kipimo cha busara na uwezo wa kusimamia mambo katika klabu ya Simba, kwetu tunadhani kipimo kimojawapo ni hiki na tungependa kuona viongozi wanasimama imara kuhakikisha Simba inarudi kwenye mstari.
Bado tunaamini kufungwa na Coastal na Toto si sababu ya kufifisha safari ya Simba katika mbio za kutwaa taji la Ligi Kuu Bara, bado kuna mechi zilizobaki ambazo zinaweza kuja na matokeo tofauti.
Kitendo cha wachezaji kupigana ni cha aibu lakini kwa kuwa kimeshatokea ni wajibu kwa viongozi wa Simba kukaa chini na wachezaji wao ili kuhakikisha wanakuwa kitu kimoja.
Tunasema hivyo tukiwa hatuamini kama ndoto za kutwaa taji la Ligi Kuu Bara zimeyeyuka baada ya timu hiyo kushindwa kutamba mbele ya Toto.
Tunajua kwamba kipigo hicho kimewaumiza wanachama na mashabiki wa Simba lakini hali hiyo isiwe sababu ya kuvuruga amani ndani ya Simba na kuondoa mshikamano ambao ulianza kuonekana wakati timu ikipata ushindi mfululizo.
Viongozi Simba ndio wenye jukumu la kuhakikisha kipigo katika mechi dhidi ya Toto hakiwi chanzo cha mifakarano na kuvuruga mipango mizuri iliyoanza kuonekana Simba.
Kama viongozi watakubali Simba iingie katika mgawanyiko kwa sababu tu timu yao imefungwa na Toto hiyo itakuwa aibu kubwa.
Hata kama kuna madai ya baadhi ya wachezaji kuihujumu Simba ni muhimu utafiti ufanywe kwa lengo la kuhakikisha ukweli unajulikana ili kama ni kuadhibiwa basi iwe ni adhabu itakayozingatia misingi ya haki.