Kwa mwendo huu, Azam imepania asee!

MATAJIRI wa Azam FC hawataki masikhara kabisa awamu hii ana kwa namna usajili wao unavyokwenda, timu nyingine nchini zijipange kweli kweli.

Mabingwa hao watetezi wa Kombe la Kagame, tayari wamemsainisha kiungo wao, Mudathir Yahya, mkataba mpya wa miaka miwili huku wakiwanasa pia Tafadzwa Kutinyu, Ditram Nchimbi, Donald Ngoma, Nicolas Wadada pamoja na kuimarisha benchi la ufundi kwa kumchukua kocha Hans Pluijm akitokea katika kikosi cha Singida United.

Lakini licha ya kufanya usajili huo, kigogo mmoja wa juu kutoka ndani ya klabu hiyo ameliambia Mwanaspoti kuwa hizo ni mvua za rasharasha tu kwani za masika ndio zinakuja.

“Tulipokea mapendekezo ya kocha mapema na kutuambia sehemu ambazo anataka afanyiwe marekebisho ndio maana tumefanya hivyo, tutazidi kusajili kadiri maelekezo ya kocha yanavyoelekeza,” alisema kigogo huyo.

Baada ya timu hiyo kufanikiwa kudaka saini ya Nicolas Wadada anayecheza nafasi ya beki wa kulia, habari za chinichini zilianza kwamba usajili huo umepoteza mpango wa kumchukua beki Juma Abdul wa Yanga ambaye alikuwa akihitajika na kikosi hicho kwa muda mrefu.

Lakini kigogo huyo aliliambia Mwanaspoti, wanahitaji kuwa na wachezaji wazuri wanaocheza nafasi moja ili kuhakikisha kuna kuwa na changamoto kwa wachezaji ili timu iweze kufanya vizuri.

“Tunataka tuwe na kikosi kipana chenye ushindani kwa wachezaji, ukiwa na wachezaji ambao wanapeana ushindani wao kwa wao timu itafanya vizuri, kwa hiyo ishu ya Abdul bado ipo lakini tusubili muda ndio utakaoamua kwenye kipindi hiki cha usajili,” aliongeza kusema kigogo huyo.