Cavani hatihati kuikosa Ufaransa

Muktasari:
Mmoja wa maofisa wa Uruguay alisema Cavani aliyeumia katika mchezo uliopita wa hatua ya 16 bora dhidi ya Ureno, bado hajawa fiti na madaktari wanamuangalia kwa karibu.
Moscow, Russia. Mshambuliaji wa Uruguay, Edinson Cavani ana uwezekano mkubwa wa kuukosa mchezo wa kesho wa robo fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Ufaransa kutokana na kuwa majeruahi.
Mmoja wa maofisa wa Uruguay alisema Cavani aliyeumia katika mchezo uliopita wa hatua ya 16 bora dhidi ya Ureno, bado hajawa fiti na madaktari wanamuangalia kwa karibu.
Mchezaji huyo mwenye miaka 31 alikosa mazoezi ya timu hiyo kwa siku ya tatu mfululizo akiuguza mguu wake wa kushoto uliopata majeraha, kabla ya jana kuanza kufanyishwa mazoezi mepesi ya kumuweka fiti.
Cavani anayekipiga kwenye klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa alifunga bao moja katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Ureno, uliowawezesha kutinga robo fainali, lakini aliumia na kutolewa uwanjani dakika ya 74.
Kutokana na hatihati hiyo kocha wa Uruguay, Oscar Tabarez, alisema jana mshambuliaji wa Girona, Christian Stuani atachukua nafasi ya Cavani katika kikosi kitakachoanza kesho.
Tabarez alisema kukosekana kwa Cavani kutamlazimisha kubadili mfumo ambapo itabidi wamtumie mshambuliaji mmoja mbele Luis Suarez.