#WC2018: WAMETISHA Wafungaji wa mabao ya kwanza mechi za kwanza Kombe la Dunia

Muktasari:
- Wafuatao ni mastaa ambao waliingia katika rekodi ya kuwa wafungaji wa mabao ya kwanza ya michuano hii maarufu duniani.
MOSCOW, RUSSIA. KAMA kuna raha kubwa katika fainali za Kombe la Dunia basi ni kuingia katika rekodi ya kuwa mfungaji wa bao la kwanza la michuano hiyo mikubwa.
Wafuatao ni mastaa ambao waliingia katika rekodi ya kuwa wafungaji wa mabao ya kwanza ya michuano hii maarufu duniani.
Omam-Biyik (Argentina vs Cameroon, 1990)
KATIKA pambano hili la kwanza la Kombe la Dunia 1990 lililochezwa Uwanja wa San Siro jijini Milan, Cameroon iliwashangaza mashabiki wa soka duniani kote kwa kuwafunga mabingwa watetezi Argentina bao 1-0. Bao hili lilifungwa katika dakika ya 67 ya mchezo na mshambuliaji, Francois Omam-Biyik ambaye aliruka kwa kichwa na kufunga bao hilo pekee.
Katika pambano hilo, wachezaji wawili wa Cameroon, Benjamin Masing na mdogo wake Omam-Biyik, Andre Kana Biyik walitolewa nje kwa kadi nyekundu. Argentina waliokuwa chini ya Diego Maradona walitoka vichwa chini kwa aibu huku Biyik akiingia katika historia ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao fainali za mwaka 1990
Jurgen Klinsmann (Ujerumani vs Bolivia, 1994)
Katika pambano hili lililochezwa Juni 17, 1994 katika Uwanja wa Soldier Field jijini Chicago, Ujerumani ambao walikuwa mabingwa watetezi wa michuano hiyo hawakutaka kufuata nyayo za Argentina. Licha ya ugumu walioupata katika safu ya ulinzi ya Bolivia lakini hatimaye katika dakika ya 61 ya pambano hilo staa wao, Jurgen Klinsmann alifanikiwa kuziona nyavu za Bolivia. Bao hilo lililkuwa la kwanza la michuano hiyo ingawa baadaye Ujerumani walishindwa kutetea taji lao.
Cesar Sampaio (Brazil vs Scotland, 1998)
Hizi zilikuwa fainali za Zinedine Zidane lakini kabla ya michuano hiyo kuanza jina la Ronaldo de Lima lilitawala zaidi. Hata hivyo, katika mechi ya kwanza Ronaldo hakuziona nyavu na badala yake mfungaji wa bao la kwanza katika mechi ya kwanza ya michuano hii iliyofanyika nchini Ufaransa alikuwa ni mlinzi wa Brazil, Cesar Sampaio.
Ilikuwa ni katika pambano la ufunguzi dhidi ya Scotland katika Uwanja wa taifa wa Ufaransa Stade de France. Pambano hilo lilimalizika kwa ushindi wa mabao 2-1 kwa Brazil.
Hata hivyo, katika pambano la fainali dhidi ya Ufaransa, Brazil walishindwa kuonyesha makali yao baada ya kuchapwa mabao 3-0 shukrani kwa mabao mawili ya vichwa ya Zidane huku Emmanuel Petit akimalizia bao la tatu katika dakika za majeruhi.
Papa Diop (Ufaransa vs Senegal, 2002)
Kwa mara ya kwanza katika historia michuano hii ilifanyika katika nchi mbili tofauti. Ilifanyika katika nchi za Korea Kusini na Japan. Wakati pambano la ufunguzi lilichezwa katika jiji la Seoul nchini Korea Kusini, pambano la fainali lilifanyika jijini Yokohama Japan.
Maajabu ya timu ndogo ya Afrika kuifunga timu kubwa duniani yaliendelea katika michuano hiyo. Senegal walifuata nyayo za Cameroon za mwaka 1990 baada ya kuwaduwaza mabingwa watetezi Ufaransa kwa ushindi wa bao 1-0.
Bao pekee la ushindi ambalo lilikuwa bao la kwanza la michuano hiyo lilifungwa na kiungo, Papa Bouba Diop. Wakati bao la kwanza lilifungwa Korea Kusini na Diop, bao la mwisho la michuano lilifungwa nchini Japan katika pambano la fainali kati ya Brazil na Ujerumani, Ronaldo de Lima alifunga mabao mawili katika ushindi wa mabao 2-0 wa Brazil dhidi ya Ujerumani iliyotwaa kombe.
Phillip Lahm (Ujerumani vs Costa Rica)
Mfumo wa timu mwenyeji kucheza pambano la ufunguzi ulianzia hapa. Katika pambano hili wenyeji UJerumani walianza kwa kutoa onyo katika mechi ya ufunguzi baada ya kuichapa Costa Rica mabao 4-2 huku mlinzi Phillip Lahm akifunga bao la kwanza la michuano hiyo katika dakika ya tano tu ya mchezo.
Baadaye Miroslav Klose alifunga mabao mawili huku Torsten Frings akifunga bao moja. Mabao ya Costa Rica yote mawili yalifungwa na staa wao, Paulo Wanchope. Kwa idadi ya mabao sita katika mechi hiyo pambano hilo liliweka rekodi ya mechi ya ufunguzi iliyofungwa mabao mengi zaidi katika historia.
Hata hivyo wenyewe Ujerumani hawakuweza kutumia vema uenyeji wao kutwaa taji hilo na badala taji lilikwenda kwa Italia ambao waliifunga Ufaransa kwa matuta katika pambano la fainali.
Siphiwe Tshabalala (Afrika Kusini vs Mexico, 2010)
Kwa mara ya kwanza michuano hii ilifanyika katika Bara la Afrika. Katika hali ya kupendeza zaidi Mwafrika alifunga bao la kwanza katika michuano hiyo. Katika pambano la ufunguzi katika ya Afrika Kusini dhidi ya Mexico dimba la Soccer City, staa wa Bafana Bafana, Siphiwe Tshabalala alifanikiwa kuwanyanyua mashabiki wa bara zima la Afrika baada ya kufunga bao la kuongoza katika dakika ya 56 ya pambano hilo.
Hata hivyo Waafrika walirudishwa vitini kwa bao safi ya kusawazisha lililofungwa na mlinzi mkongwe wa Mexico, Rafael Marquez. Haikuwa fainali nzuri kwa wenyeji kwa sababu waliishia katika hatua ya makundi tu.
Marcelo (Brazil vs Croatia, 2014)
Kwa mara ya kwanza bao la ufunguzi la michuano ya Kombe la Dunia lilikuwa la kujifunga. Ilikuwa ni katika fainali za mwaka 2014 na Brazil walicheza mechi yao ya kwanza ya ufunguzi dhidi ya Croatia jijini Sao Paulo lakini mlinzi, Marcelo akajifunga katika dakika ya 11 tu ya mchezo.
Hata hivyo, staa wa Brazil, Neymar alifanikiwa kufuta makosa kwa kufunga mabao mawili huku moja likiwa la penalti kabla ya Oscar kufunga bao la tatu katika dakika ya 90.
Hata hivyo, hazikuwa fainali nzuri kwa wenyeji ambao kwa mara ya kwanza katika historia ya kombe la dunia walipata kipigo cha aibu baada ya kucharazwa mabao 7-1 na Ujerumani katika pambano la nusu fainali. Ujerumani walikwenda kutwaa taji hilo.
Yury Gazinsky (Russia vs Saudi Arabia, 2018)
Katika michuano hii ya mwaka huu, juzi staa wa Russia, Yury Gazinsky aliingia katika rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga bao katika fainali za Kombe la Dunia za mwaka huu.
Kama vile haitoshi, baada ya ushindi wa mabao 5-0 wa Russia dhidi ya Saudi Arabia, ushindi huo nao umeingia katika rekodi ya kuwa miongoni ya mechi ya ufunguzi yenye mabao mengi zaidi baada ya mechi ya ufunguzi kati ya Ujerumani na Costa Rica mwaka 2006.
Haijulikani kama Russia itaweza kufanya maajabu ya kufika mbali au kuchukua taji lenyewe wakiwa kama wenyeji.