#WC2018: Marcelo ni ‘Roberto Carlos’ mwenye wigi lake Russia

Muktasari:
Ndiyo, katika timu nyingi za taifa, kuanzia mashabiki, makocha, vyombo vya habari, pamoja na wachezaji wenyewe huwapa umuhimu mkubwa sana baadhi ya wachezaji kuwa msaada mkubwa katika mafanikio ya timu kuliko wengine ambao kimsingi huwa ndio kama injini au mafuta kwenye injini.
UMEBAKI mwezi mmoja tu, makocha na mabenchi ya ufundi ya kila taifa kwa sasa vichwa vyao vinawaka moto, ile panga pangua si unajua inavyoletaga mijadala? Hakuna kuoneana aibu sasa, mwenye kiwango aende asiyekuwa fiti apishe wengine.
Ndiyo, katika timu nyingi za taifa, kuanzia mashabiki, makocha, vyombo vya habari, pamoja na wachezaji wenyewe huwapa umuhimu mkubwa sana baadhi ya wachezaji kuwa msaada mkubwa katika mafanikio ya timu kuliko wengine ambao kimsingi huwa ndio kama injini au mafuta kwenye injini.
Leo tuiangalie Selecao, hivi wangapi watakuwa wanaliimba jina la Neymar, sijui Coutinho, Jesus, Firminho, Fenandinho au Casemiro? Ninaona kama wote hivi. Lakini je, nikiulizia huduma ya mtu mmoja ambaye anaunda ukuta mmoja imara kule nyuma, mimi namuita ‘Bambucha’ ila maarufu kama Marcelo ninadhani wachache sana watanyoosha mikono, hasa mashabiki wa Los Blancos kwa sababu wanajua shughuli yake.
Nasemaje, Marcelo ni bonge moja la mlinzi wa kileo. Huwezi kuzungumzia mafanikio ya klabu ya Real Madrid ya kuingia fainali ya Mabingwa Ulaya mara tatu mfululizo na kuchukua mara mbili kati ya hizo, bila ya kutaja jina la huyu mtu. Marcelo ni aina ya beki wa kileo ambao hupandisha mashambulizi na kushuka kusaidia kukaba. Ana kasi, anapunguza ukija kichwa kichwa, ana kontroo vyema, anapiga mashuti, anafunga pia, unapata wapi beki wa namna hii kwa dunia ya sasa?, Wapo wachache sana.
Angalia mijongeo yake akiwa uwanjani na guu lake la mavi, amekuwa na mchango mkubwa sana kwa mabao ya vichwa ya Ronaldo, na pia kucheza mipira inayorudi (rebounds) pale na Madrid inahitaji matokeo amekuwa akiibuka kama shujaa mara kadhaa. Katika mchezo dhidi ya Bayern alifunga bao muhimu lililowarudisha Madrid mchezoni, kabla ya kuongoza kupitia kwa Marco Asensio kule Allianz Arena.
Pale Madrid viatu vyake vimekuwa vigumu kuvalika, anapokuwa yuko nje. Si mchezaji wa kupata majeraha kila wakati, hana kadi za kijinga za kujitafutia, aina ya wachezaji hawa wanakuhakikishia huduma ya uhakika. Namuona Roberto Carlos mpya lakini asiye na kipara huyu yeye ana ‘wigi’ na tattoo zinazomfanya awe yeye.
Kule Brazil atakuwa mtu muhimu sana kama mwalimu atajua kumtumia, na kumuwekea watu wanaoweza kumalizia krosi majaro atakazokuwa anazipiga. Brazil ina watu wazuri mbele, Fred, Neymar, Jesus, Coutinho, au Firminho yeyote kati ya hawa watak uwa na faida kubwa ya kuwa na huyu mtu, kazi kwao washindwe wenyewe tu mwaka huu.