#WC2018: Edinson Cavani kuikosa robo fainali

Mshambuliaji nguli wa Uruguay, Edinson Cavani, ameiweka njiapanda Uruguay katika mchezo wa robo fainali dhidi ya Ufaransa.
Cavani anatarajiwa kukosa mchezo wa Ijumaa baada ya kupata maumivu makali ya mguu katika mchezo wa jana usiku dhidi ya Ureno.
Mshambuliaji huyo wa Paris Saint Germain (PSG), alitoka uwanjani akisaidiwa na nahodha wa Ureno, Cristiano Ronaldo baada ya kuumia.
Kocha Oscar Tabarez alisema Cavani hawezi kucheza mchezo huo kutokana na jeraha alilopata katika mchezo huo walioshinda mabao 2-1.
Tabarez anayembelea magongo baada ya kupata jeraha la nyonga, alisema kumkosa mshambuliaji huyo ni pigo katika kikosi chake.
Cavani aliyefunga mabao yote mawili katika mchezo huo, ataikosa Ufaransa ambayo juzi jioni iliing’oa Argentina kwa ushindi wa mabao 4-3.
“Alipata maumivu makali, sina taarifa rasmi atakuwa fiti lini kwa sababu sijazungumza na madaktari kuhusu jeraha lake, lakini tuna siku tano (nne) zijazo tutakuwa na mechi sidhani kama atakuwa amepona,” alisema Tabraez.
Kocha alisema wanaendelea kufanya uchanguzi wa jeraha ingawa matumaini ya kucheza mchezo wa Ijumaa utakuwa mdogo.
Kocha huyo alisema mchezo wa juzi usiku ulikuwa mgumu na haikuwa kazi rahisi kupata ushindi katika mchezo huo.
Mashabiki wa Uruguay wametuma maombi ya kumuombea nyota huyo kupona haraka kabla ya mchezo wa Ijumaa.
Mshambuliaji huyo amekuwa na kiwango bora katika klabu yake ya PSG akicheza pacha na nyota wa Brazil Neymar.
Mchezaji huyo mwenye miaka 31, amefunga mabao 45 katika michezo 105 aliyocheza katika kikosi cha Uruguay.