Zilizobamba 2025; Ulikuwa mwaka wa Simbu, Geay
Muktasari:
- Kwa upande wa mchezo wa riadha, tumeshuhudia wanariadha wetu wakiweka alama isiyofutika katika vitabu vya kumbukumbu kwenye mashindano mbalimbali.
MICHEZO mbalimbali imeipa heshima Tanzania kwa mwaka 2025 ambao unakwenda ukingoni.
Kwa upande wa mchezo wa riadha, tumeshuhudia wanariadha wetu wakiweka alama isiyofutika katika vitabu vya kumbukumbu kwenye mashindano mbalimbali.
Hata kama rekodi walizoweka zitakuja kuvunjwa, lakini itabaki kwamba wao walianza, kisha wengine wakafuata.
Hapa tumekuchambulia baadhi ya matukio makubwa yaliyofanywa na wanariadha wa Kitanzania katika nyanja ya kimataifa kwa mwaka 2025.
BALAA LA SIMBU
Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, Alphonce Simbu kuna mambo matatu makubwa ameyafanya mwaka 2025 na kuacha alama ya heshima nchini.
Kwanza alikwenda Marekani kushiriki mbio za Boston Marathon zilizofanyika Aprili 21, 2025 jijini Boston na kumaliza wa pili kwa muda wa 2:05:04 na kuwa Mtanzania wa pili ambaye amewahi kumaliza mbili bora kwa mbio hizo baada ya Gabriel Geay kufanya hivyo mwaka 2023.
Nyota huyo kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakati anamaliza wa pili kwa muda wa 2:05:04, Mkenya John Korir aling'ara kwa kushika nafasi ya kwanza kwa muda wa 2:04:05.
Nafasi ya tatu ilikwenda kwa Cybrian Kotut wa Kenya ambaye ametumia muda wa 2:05:08 huku mwenyeji Conner Mentz wa Marekani akimaliza wa nne kwa kutumia saa 2:05:08.
Baada ya hapo, Simbu akaweka rekodi na historia ya kuwa Mtanzania wa kwanza kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya dunia ya riadha 2025 yaliyofanyika Septemba 15, 2025 jijini Tokyo, Japan.
Simbu alimaliza mbio ndefu za marathoni za kilomita 42 katika joto na unyevunyevu mkali na kutwaa ubingwa huo kwa wanaume na iliamuliwa kwa tofauti ndogo zaidi katika historia ya mchezo huo dhidi ya aliyeshika nafasi ya pili, Mjerumani Amanal Petros.
Ushindi huo wa kishindo umemfanya Simbu aingie katika vitabu vya kumbukumbu kama mwanariadha wa kwanza wa Tanzania kushinda dhahabu katika riadha za dunia.
Katika ushindi huo ulioamuliwa kwa pengo dogo zaidi kuwahi kushuhudiwa katika historia ya marathoni za mashindano ya dunia, mshindi alitenganishwa kwa sekunde 0.03 pekee.
Simbu alitwaa medali hiyo ya dhahabu katika mashindano ya 25 ya dunia nchini humo akitumia saa 2:09:48, akatofautiana sekunde 0.03 na mshindi wa pili, Amanal Petros wa Ujerumani, huku Iliass Aouani wa Italia aliyetumia saa 2:09:53 akihitimisha tatu bora.
Mwisho kabisa, Novemba 30, 2025, Simbu alikuwa Ufaransa kwa ajili ya kushiriki sherehe za tuzo za wanariadha bora wa mwaka 2025 zilizoandaliwa na shirikisho la riadha la dunia.
Hafla hiyo ilifanyika jijini Monaco, kwa kuwakutanisha wanariadha 12 walioteuliwa kushindania tuzo katika vipengele mbalimbali, Simbu akiwa ni miongoni mwao.
Nyota huyo wa mbio ndefu (marathoni), aliwania tuzo ya mwanariadha bora wa mbio za nje ya uwanja kwa wanaume, dhidi ya Sebastian Sawe wa Kenya, baada ya wawili hao kupenya mchujo mkali uliowahusisha makundi tofauti ya wanariadha duniani. Simbu alishindwa na Mkenya huyo.
Licha ya kutokuwa mshindi, hata hivyo, Simbu ameandika historia kwa kuwa Mtanzania wa kwanza kufika hatua hiyo ya juu katika tuzo za dunia tangu Tanzania ilipoanza kuishiriki mashindano ya riadha ya dunia mwaka 1983.
GEAY AKINUKISHA KIMATAIFA
Kwa upande mwingine, mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, Gabriel Geay alianza kushiriki mbio za Aramco Huston Half Marathoni za Marekani zilizofanyika Januari 19, 2025 na alishika nafasi ya tatu kwa muda wa 59:18.
Muda huo ulimfanya kuvunja na kuweka rekodi mpya ya taifa ya nusu marathoni iliyodumu kwa miaka saba tangu ilipowekwa mwaka 2017 na marehemu Ismail Juma kwa muda wa dakika 59:30 katika mbio za nusu marathoni za Jamhuri ya Czech.
Pia Geay alishinda mbio za Daegu Marathon 2025, zilizofanyika Februari 23, 2025, Korea Kusini huku akiweka rekodi mpya.
Geay ambaye alimaliza wa pili katika mbio za Boston Marathon za 2023 za Marekani, alimshinda Shujaa wa Ethiopia ambaye aling’ara Dubai Marathon 2024, Addisu Gobena na kutwaa ushindi wake wa kwanza wa mbio hizo akitumia muda wa 2:05:20 na kuweka rekodi mpya ya mwanariadha ambaye ametumia muda mchache katika mbio hizo kwa upande wa Wanaume.
Addisu alimaliza wa pili kwa muda wa 2:05:22 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Mwiethiopia mwenzake Dejene Magersa kwa muda wa 2:05:59.
MOTO ALIOUWASHA MAGDALENA SHAURI
Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania na bingwa wa marathon taifa upande wa wanawake, Koplo Magdalena Shauri alikwenda Marekani kushiriki mbio za Chicago Marathon.
Mbio hizo zilifanyika Oktoba 12, 2025 jijini Chicago na Magdalena alimaliza wa tatu kwa muda wa 2:18:03 na kuwa Mtanzania wa kwanza kumaliza tatu bora katika mashindano hayo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1977.
Nyota huyo ambaye alikuwa anashikilia rekodi ya taifa ya muda wa saa 2:18:41 aliyoiweka mwaka 2023 kwenye Berlin marathon, alionyesha ubora na uthabiti mkubwa kwa kuivunja, huku akiiboresha kwa sekunde 38, kutoka masaa 2:8:41 hadi 2:18:03.
REKODI YA NEEMA MSUADI
Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania, Neema Msuadi alikwenda Urusi kushiriki mbio za Perm Marathon.
Mbio hizo zilifanyika Oktoba 2025 jijini Perm ambapo Neema alimaliza wa kwanza kwa muda wa 2:38:15, na kuwa Mtanzania wa pili kuongoza katika mbio ndefu mwaka huu baada ya Gabriel Geay kufanya hivyo mapema Februari 2025 akishinda Daegu Marathon za Korea Kusini kwa muda wa 2:05:20.
WANARIADHA SITA WAFANYA KWELI NAGAI CITY
Wanariadha sita walioiwakilisha Tanzania katika mbio za Nagai City Marathon za Japan zilizofanyika Oktoba 19, 2025 katika mji wa Nagai, waliing'arisha nchi kwa kufanya kweli.
Wanariadha hao katika mbio zote walizoshiriki Marathon KM 42 na nusu marathoni KM 21, wanaume na wanawake, walimaliza nafasi nne za juu, KM 42 wanaume, Michael Sanga akishika nafasi ya kwanza kwa muda wa 2:15:26, Charles Sulle akamaliza wa pili kwa muda wa 2:16:30 huku Vaileth Kidas akitumia muda wa 2:41:37, upande wa Wanawake.
KM 21, Joseph Panga alimaliza wa pili kwa muda wa 1:02:52 huku Jumanne Ndege akimaliza wa nne kwa muda wa 1:06:07, wakati Agnes Mwaghui akishinda kwa upande wa wanawake baada ya kutumia muda wa 1:12:51.